Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WANACHAMA wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wilayani Mbinga
mkoa wa Ruvuma, wametakiwa kuacha malumbano miongoni mwao badala yake wajenge mshikamano
na kuwa pamoja, ili waweze kusonga mbele kimaendeleo.
Aidha imeelezwa kuwa endapo wataendekeza hali hiyo, majungu
na fitina hayatawafikisha mbali ndani ya umoja huo jambo ambalo litasababisha
waendelee kufarakana na kujenga makundi ambayo yatawagawa na kuleta mpasuko
kati yao.
Rai hiyo ilitolewa na Katibu wa UWT wilaya ya Mbinga, Martina
Katyale alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, juu ya
maendeleo ya Umoja huo wa wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani hapa.
Katibu huyo alieleza kuwa wakati umefika sasa kwa wanawake wilayani
humo, kujishughulisha na kazi za ujasiriamali ili waweze kuepukana na mambo
hayo na kuwafanya wakue kiuchumi, kutoka ngazi ya familia zao na chama kwa
ujumla.
“Nawasihi wanawake wenzangu tuachane na tabia ya
kutengenezeana maneno ya hapa na pale ambayo hayatatujenga, mifarakano au matatizo
yoyote yale yanayojitokeza katika jamii, hayawezi kuleta amani bali hujenga
chuki na kuondoa upendo miongoni mwetu”, alisema Katyale.
Katyale alisisitiza kwamba wanachotakiwa wajiulize kwanza
wametoka na wanakwenda wapi, huku wakiacha tabia za unafiki na uongo vitendo
ambavyo kama wataviendekeza havitawafikisha mbali.
Katibu huyo wa UWT alifafanua kuwa Tanzania ni nchi ambayo
wanawake wamekuwa wakipendana, hivyo chama kilichopo madarakani hakitakubali
kuiacha rehani kwa watu wabovu ambao hawana nia njema na taifa hili.
Pamoja na mambo mengine, aliongeza kuwa Umoja huo wa Wanawake
hauendeshwi kwa mtindo kama vile wa kucheza bao, hivyo wameshauriwa kuwa makini
na majukumu ya kazi zao za kila siku katika kutumikia wananchi huku akiongeza
kwa kuwataka wanachama wenzake, kuwabeza watu ambao wakati wote wamekuwa
wakipinga maendeleo pale yanapofanyika.
No comments:
Post a Comment