Na Steven Augustino,
Tunduru.
WATU wawili ambao ni wakazi wa kijiji cha Mkapundwa wilayani
Tunduru mkoa wa Ruvuma, wamehukumiwa kutumikia kifungo cha miezi 10 jela baada
ya kupatikana na kosa la kukutwa na lita 60 za pombe ya moshi, maarufu kwa jina
la gongo.
Adhabu hiyo ilitolewa na Hakimu mfawidhi wa Mahakama ya wilaya
hiyo, Gladys Barthy baada ya mahakama hiyo kujiridhisha na ushahidi uliotolewa
na upande wa mashtaka.
Kwa mujibu wa mwendesha mashtaka mkaguzi msaidizi wa Polisi
Inspekta Songelaeli Jwagu alidai mahakamani hapo kuwa, watuhumiwa waliokuwa
wanakabiliwa na shauri hilo kuwa ni, Mohamed Ally Buji aliyehukumiwa kutumikia
kifungo cha miezi 6 au kulipa faini ya shilingi 350,000 na Mohamed Ally Mohamed
aliyehukumiwa kifungo cha miezi 4 au kulipa faini ya shilingi 250,000.
Awali akiwasomea shtaka hilo Inspekta Jwagu aliambia mahakama
hiyo kuwa watuhumiwa hao walinaswa wakiwa wanasafirisha pombe hiyo, kutoka
katika kijiji cha Mkapunda wilayani humo Oktoba 20 mwaka 2014.
Katika tukio hilo alisema, watuhumiwa hao walikiuka sheria
namba 30 ya kudhibiti pombe za kienyeji sura namba 384 ya kanuni ya adhabu kama
ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Aidha baada ya mahakama hiyo kuwatia hatiani Inspekta Jwagu
aliiomba mahakama hiyo kuwapatia adhabu kali, ili iwe fundisho kwa watu wengine
ambao wamekuwa na tabia kama hiyo.
Wote walipelekwa katika Gereza la Wilaya ya Tunduru na kuanza
kutumikia vifungo vyao baada ya kushindwa kulipa faini zao.
No comments:
Post a Comment