Na Bashir Yakub,
NI kawaida watu kukopeshana
fedha katika shughuli za kibinadamu za kila siku
hasa zile za uzalishaji. Kutokana na hili
baadhi ya watu hujikuta wameingia katika
faraka ambazo hata hivyo zinatatulika kisheria.
Kwa wale ambao madeni yao
hutokana na taasisi za fedha kama
benki hawa huwa sio rahisi kwao kukwepa
kutokana na utaratibu makini wa utoaji wa
fedha wa taasisi hizo. Tatizo kubwa la kutolipana
na kuleteana dharau huhusisha wadeni binafsi yaani
mtu na mtu. Ni katika madeni haya ya
watu binafsi ambamo msemo maarufu wa deni
halifungi husikika.
Ni kawaida kukuta mtu
amekopeshwa na hataki kurejesha akijiamini
kuwa deni halifungi. Yumkini wapambe nao
husikika wakisema, asikutishe huyo deni
halifungi. Kwa makala haya tutapata kujua
ikiwa ni kweli deni linafunga au halifungi.
1. KESI YA MADAI
Kesi za madai ni zile kesi
zote ambazo si za jinai. Kesi
za madai hazihusishi kudaiana pesa tu kama
wengi wanavyojua. Hata masuala ya talaka, kudai fidia,
mikataba, madai ya vitu kama nyumba, magari n.k
navyo huingia katika kesi za madai. Kwa
hiyo tunapojiuliza swali ikiwa deni
linafunga au halifungi tunaongelea hivi vyote.
Hata hivyo tutajielekeza zaidi katika kudaiana
fedha.
2. JE INARUHUSIWA KUPELEKA KESI
YA MADAI POLISI ?
Unayo haki ya kufungua shauri
ikiwa kuna mtu unamdai lakini kwa sharti kuwa
shauri lifunguliwe mahali husika. Wapo ambao
hupeleka kesi za namna hii polisi
japo huko si mahali pa kesi za
namna hii. Polisi hujitahidi kuzitafutia
ufumbuzi ambapo wakati mwingine hufanikiwa
na wakati mwingine hushindwa.
Ukweli ni kwamba kisheria
polisi hawana ruhusa ya kushughulikia
kesi za madai hasa hizi za
kudaiana hela na hata mali. Ni basi
tu wanaamua kuzishugulikia lakini si kazi
yao kisheria. Madhara utakayoyapata utakapomfungulia
kesi mdai wako polisi ni pamoja na
kupoteza mda bila kupata ulichokitaka. Hii
ni kwasababu mdaiwa atakapokataa kutoa
ushirikiano wowote, polisi hawana la kumfanya.
Hawawezi kumfunga kwasababu hairuhusiwi.
Hawawezi kumpeleka mahakamani kwasababu hawaruhusiwi
kupeleka kesi za madai Mahakamani. Kwahiyo
mdaiwa uliyempeleka polisi akiamua kukomaa
hawana la kufanya utakuwa umepoteza
muda na gharama.
Basi ieleweke kuwa kesi za
madai kama haya hutakiwa kufunguliwa Mahakamani.
Yaweza kufunguliwa Mahakama yoyote kutegemea
na kiwango cha fedha unachodai. Waweza
kufungua Mahakama ya mwanzo, wilaya na hata
Mahakama kuu. Usipeleke kesi ya namna hii polisi
labda kama unalenga kumtisha mdeni na
si kupata haki.
3. JE DENI HALIFUNGI KISHERIA?
Hapana, deni linafunga. Ikiwa
utashitakiwa kwa kudaiwa fedha na
hukumu ikatolewa kuwa unatakiwa kulipa hizo
fedha basi unatakiwa uzilipe. Ikiwa hauna
basi itaangaliwa kama una mali kama
nyumba, gari au mali yoyote ambayo inaweza
kukamatwa ili kulipia deni. Ikiwa hauna nyumba,
gari au mali nyingine yoyote inayoweza
kufidia deni basi itatakiwa ukamatwe
ufungwe kwa ajili ya deni hilo.
Kifungu cha 44 ( 1 ) cha sheria ya
mwenendo wa mashauri ya madai kinasema kuwa
mdaiwa anaweza kukamatwa katika muda na
siku yoyote na haraka
kufikishwa Mahakamani na kwamba Mahakama
inaweza kutoa amri ya kuwekwa kizuizini/kufungwa.
Kwa hiyo deni linafunga labda mdai
asiamue kuchukua hatua.
4. JE UKIFUNGWA DENI LINAISHA ?
Hapana ukifungwa deni haliishi.
Kifungu cha 46 ( 2 ) cha sheria ya mwenendo
wa mashauri ya madai kinasema kuwa
mdaiwa aliyeondolewa katika kifungo kwa sababu
yoyote ile, iwe kwa kumaliza muda, ugonjwa
au vinginevyo hatahesabika kuwa ameondolewa
katika deni kutokana na kuachiwa huko.
Hii ina maana unatumikia kifungo
kikiisha deni linabaki palepale.
Kifungo hakifuti au kusimama
badala ya deni isipokuwa ni adhabu ya
ukorofi. Ni kutokana na mtazamo huo wa sheria
unaolazimisha kutakiwa kulipa deni hata baada ya
kutumikia kifungo. Ukishindwa mara nyingine tena
kulipa mdai anayo haki ya kukurudisha tena
Mahakamani ambapo unaweza kufungwa tena. Msimamo
wa sheria ni mpaka ulipe tu.
5. KULIPIWA DENI UKIWA JELA
Muda wowote mdaiwa akiwa jela
anatumikia adhabu yake ya deni anaweza
kuondolewa na kufutiwa adhabu hiyo iwapo
kiwango cha deni analodaiwa kitalipwa.
Mahakama iliyotoa amri ya kufungwa
ndiyo itakayotoa amri ya kuachiwa baada ya deni kulipwa
katika ukamilifu wake.
MWANDISHI WA MAKALA
HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI
WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA SERIKALI
LA HABARI LEO KILA JUMANNE, GAZETI
JAMHURI KILA JUMANNE NA GAZETI
NIPASHE KILA JUMATANO.
0784482959,
0714047241 bashiryakub@ymail.com
No comments:
Post a Comment