Sunday, December 20, 2015

TUNDURU KUSHTAKIWA KWA RAIS MAGUFULI




Na Steven Augustino,
Tunduru.

DIWANI wa Kata ya Mlingoti Mashariki, Mohamed Aloyce kupitia Chama Cha Wananchi (CUF) amepanga kuwashtaki kwa Rais Dokta John Pombe Magufuli, viongozi wa Halmashauri ya wilaya Tunduru mkoani Ruvuma, juu ya ubabaishaji unaofanywa na kushindwa kusimamia kikamilifu soko la ununuzi wa zao la korosho kutoka kwa wakulima wilayani humo.

Mohamed alitoa kauli hiyo wakati alipokuwa akizungumza na mamia ya wakulima wa zao hilo, katika vituo vya kuuzia korosho  Chama cha msingi Mlingoti  (AMCOS) vilivyopo katika kata yake na kwamba, hali hiyo imetokana na kubaini uwepo wa nia mbaya kwa viongozi hao kutaka kujinufaisha wao binafsi kupitia mgongo wa wakulima.

Rais Dokta John Magufuli.
Akifafanua taarifa hiyo, Aloyce alisema kuwa kinachomshangaza yeye na madiwani wengine ni kwamba mamlaka waliyojikabidhi viongozi hao wa Halmashauri, wamefikia hatua ya kuruhusu makampuni mawili tu, kati ya 16 ambayo yaliomba kununua zao hilo katika msimu wa mwaka 2015/2016.

Katika taarifa hiyo aliyataja makampuni mawili yaliyoruhusiwa kununua korosho kuwa ni kampuni ya Export Trading Company Limited na Chama kikuu cha ushirika cha wilaya ya Tunduru (TAMCU) na kwamba kutokana na hali hiyo, inaonesha wazi kuwa viongozi hao hawapo tayari kufanya kazi kwa kuruhusu soko huria na makampuni mengine yaweze kununua zao hilo, ili kuweza kuleta ushindani katika soko huria na wakulima waweze kunufaika nalo.


Alisema wanamuomba Rais Magufulia kuingilia kati juu ya suala hilo, kwa kile walichoeleza kuwa kuruhusu makampuni hayo mawili kunaisababishia hata Halmashauri yao, kukosa mapato ambayo hutokana na ushuru wa zao hilo.

“Lakini pia kwa kitendo hiki, upo uwezekano wa serikali na Halmashauri yetu kushtakiwa na makampuni mengine ambayo yalilipia leseni zao na kupewa kibali kutoka bodi ya korosho, kwa ajili ya kununua zao hili na sasa wamenyimwa fursa ya kuvifanyia kazi”, alisema Aloyce.

Awali wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi waliokutwa wakiwa wamepanga foleni kwa ajili ya kutaka kuuza korosho ni pamoja na Bimwana Mohamed na Sofia Omar kutoka kijiji cha Mchomoro, kata ya Mchangani walisema kwamba hivi sasa wanalazimika kutembea umbali mrefu kufuata maeneo ya masoko ya zao hilo bila mafanikio, jambo ambalo limeanza kuwakatisha tamaa ya kuendelea na kilimo cha zao hilo katika msimu ujao hivyo walishauri ni vyema makampuni mengine yakaruhusiwa, ili waweze kuuza korosho zao karibu na maeneo yao wanayoishi.

Nao baadhi ya viongozi wanaoshughulika na upimaji wa mazao ya wakulima kwa ajili ya kuyanunulia makampuni hayo, walisema hivi sasa wamekuwa wakilazimika kukaa majumbani na kulala mapema ili kukimbia vipigo kutoka kwa wakulima ambao walikubali kupima mazao yao, na kuyahifadhi katika maghala yao.

Walidai kwamba hivi sasa wanaishi katika hofu ya kuogopa kuibiwa kwa mazao ya wakulima hao, jambo ambalo linaweza kuwasababishia matatizo makubwa kati yao na wakulima hao.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Tunduru, Tina Sekambo wakati akijibu hoja za baadhi ya madiwani wakati wa kikao kilichoketi hivi karibuni Disemba 7 mwaka huu, alisema maamuzi ya kuruhusu makampuni hayo mawili kununua korosho kutoka kwa wakulima katika msimu wa mwaka 2015/2016 yalitolewa na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo.

Sekambo ambaye alikuwa akijibu swali kutoka kwa Diwani wa kata ya Marumba, Msenga Said Msenga aliyehoji juu ya uhalali wa viongozi hao kuruhusu makampuni mawili tu wilayani humo, kununua korosho zote kutoka kwa wakulima mbali na kugoma kuzungumzia jambo hilo katika kikao hicho, alidai kuwa baada ya kamati hiyo kupitisha maamuzi hayo pia yalipatiwa baraka na uongozi husika ngazi ya mkoa wa Ruvuma.

No comments: