Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
SERIKALI mkoani Ruvuma, imesema Diwani anayefikiri ameingia
madarakani kwa lengo la kupata utajiri ni vyema ajiondoe mapema, kwani
haitaweza kumvumilia mtu wa namna hiyo na endapo atabainika mwisho wa siku atachukuliwa
hatua na kuondolewa madarakani.
Aidha imefafanuliwa kuwa wengi wao waliongia madarakani
kupitia cheo cha udiwani, wanafikiri ndio njia pekee ya kuendekeza vitendo vya
rushwa na ufisadi katika kuhujumu miradi ya wananchi, kwa lengo la kujinufaisha
wao binafsi.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu alitoa rai hiyo leo
alipokuwa akihutubia baraza la kwanza la Madiwani wa Halmashauri ya mji wa Mbinga
mkoani humo, ambalo liliketi katika ukumbi wa Umati uliopo mjini hapa.
Said Mwambungu, Mkuu wa mkoa wa Ruvuma. |
Mwambungu alikuwa akiwasilisha salamu za serikali katika
baraza hilo, ambapo aliwataka pia Watendaji wa serikali kushirikiana pamoja na
madiwani hao ili kuweza kufikia malengo ya kimaendeleo, yaliyokusudiwa kwa
manufaa ya jamii.
“Ndugu zangu kiongozi ambaye ni mpenda rushwa au fisadi
aliyekubuhu, tukikubaini tutakuchukulia hatua na mwisho wa siku tutakuondoa,
tafuteni maisha kwa njia zilizohalali acheni kujihusisha na matendo maovu”,
alisisitiza Mwambungu.
Alieleza kuwa ili Halmashauri ya mji huo na mkoa wa Ruvuma
kwa ujumla, uweze kupiga hatua mbele ya kimaendeleo, viongozi wanawajibu wa
kudhamiria kuwatendea haki wananchi ili mwisho wa siku jamii iwakumbukwe kwa
mema na sio mabaya.
“Hapa na maanisha kwamba kila ngazi itekeleze wajibu wake,
mapato yatumike kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa, hatutamsamehe wala kujenga
huruma kwa mtu ambaye ni mwizi, na mwenye lengo la kutaka kuturudisha nyuma
kimaendeleo”, alisema.
Kadhalika Mkuu huyo wa mkoa aliongeza kuwa, lengo la serikali
ni kutaka kwenda na kasi ambayo inaendana na weledi, uaminifu na uadilifu wa
hali ya juu katika utendaji kazi kwani wakati nchi hii inapata Uhuru, Hayati
Mwalimu Julius Nyerere alisema kila mtu ni lazima afanye kazi kwa faida ya
Taifa hili.
Vilevile Mwambungu hakuwa mbali kwa kuwataka viongozi na
wananchi kwa ujumla, kuzingatia masuala ya usafi katika maeneo yao wanayoishi
na kwamba Ofisi yake hapa mkoani Ruvuma, imejiwekea utaratibu kwamba kila
Jumamosi ya mwisho wa mwezi ni siku ya kusafisha mazingira.
Awali kabla ya Mkuu huyo wa mkoa kutoa salamu hizo kwa baraza
hilo la Madiwani wa Halmashauri ya mji wa Mbinga, ulifanyika uchaguzi wa kumpata
Mwenyekiti, Makamu wake na kamati mbalimbali za halmashauri hiyo.
Kwa nafasi ya Mwenyekiti ilichukuliwa na diwani wa kata ya
Myangayanga, Ndunguru Kipwele kutoka tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliyepata
kura (24) huku akimbwaga chini mpinzani wake wa Chama Cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA), Frank Mgeni kutoka kata ya Mbinga mjini ‘B’ kwa kupata kura
2.
Nafasi ya makamu Mwenyekiti ilinyakuliwa na wa CCM kutoka
kata ya Kikolo, Tasilo Ndunguru aliyepata kura 23 na kumwacha mbali mgombea
mwenzake wa CHADEMA, Aidan Nombo wa kata ya Utiri kwa kura 3.
No comments:
Post a Comment