Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
MKURUGENZI Mtendaji Halmashauri wilaya ya Mbinga vijijini
mkoani Ruvuma, Venance Mwamengo amewaagiza watendaji wa vijiji na kata wilayani
humo kutoa elimu kwa wananchi juu ya ujenzi wa vyoo bora vya kisasa, ili waweze
kuepukana na magonjwa mbalimbali ya mlipuko.
Agizo hilo lilitolewa na
Mkurugenzi huyo, baada ya kubaini ujenzi wa vyoo hivyo katika wilaya
hiyo maeneo ya vijijini umekuwa ni wa kiwango cha chini, ambao hauzingatii
usafi wa mazingira kwa afya ya binadamu.
Rais wa Tanzania, John Magufuli. |
“Naagiza kuanzia sasa, watendaji wote ndani ya wilaya hii elimisheni
wananchi wajenge vyoo bora vya kisasa, hili suala la usafi sio hiari nataka
watu walitekeleze kwa vitendo ili tulinde afya zetu”, alisema Mwamengo.
Mwamengo alitoa rai hiyo leo, alipokuwa katika kata
mbalimbali wilayani humo kwenye zoezi la kushiriki na kuhamasisha watu kufanya
usafi ambalo linaenda sambamba na maadhimisho ya miaka 54 ya Uhuru wa Tanzania
bara hapa nchini.
Alipokuwa katika kata ya Maguu, Mkurugenzi huyo aliweza pia
kutoa onyo kali kwa mfanyabiashara Steven Haulle ambaye anauza bidhaa
mbalimbali katika jengo moja lililopo karibu na soko la kata hiyo, ambapo
alimpatia siku saba ahakikishe anakarabati choo chake ambacho mfumo wa maji
taka na shimo lake la kuhifadhia taka hizo, lilikuwa limebomoka huku likitoa
harufu jambo ambalo ni hatari kwa afya ya mtumiaji na watu wengine,
wanaozunguka katika eneo hilo.
Wakati anatoa onyo hilo, aliutaka uongozi wa kata hiyo
kumpatia taarifa kamili ya utekelezaji wa agizo hilo na endapo mfanyabiashara
huyo hatatekeleza achukuliwe hatua za kisheria, ikiwemo kulipa faini ya
shilingi 50,000 au kufikishwa Mahakamani.
“Ndugu yangu usipotimiza hili, funga shughuli za biashara yako
kabla hatujachukua hatua nyingine mbele, nasisitiza kwenu viongozi wa kata zoezi
hili ni endelevu hamasisheni wananchi wafanye usafi kuanzia majumbani kwao, ikiwemo
na ujenzi wa vyoo bora”, alisema.
Zoezi hilo la kuhamasisha wananchi kutekeleza suala la usafi
hapa katika wilaya ya Mbinga vijijini, lilianza mapema Desemba Mosi mwaka huu
ambapo mwandishi wetu ameshuhudia wananchi katika maeneo mbalimbali wilayani
humo wakihamasika kuzoa taka ngumu, kuchimba mashimo ya kuhifadhia taka hizo na
baadaye huziteketeza kwa kuchoma moto.
Katika kata ya Mapera, akina mama na wazee wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) katika kata hiyo nao walikuwa wamevalia sare za chama hicho
huku wakijigawa katika makundi na kushiriki kufanya usafi katika maeneo ya
shuleni, kituo cha afya Mapera na majumbani kwao.
Vilevile kijiji cha Nyoni wilayani humo, mwandishi wa habari
hizi alishuhudia Mwenyekiti wa kijiji hicho, Aghaton Lupogo akiwa anaongoza
kundi la watu wakifanya usafi kwa pamoja katika eneo wanalofanyia mnada kijijini
hapo ambalo lilikuwa limeshamiri uchafu wa taka ngumu, ambapo walikuwa
wakizikusanya na kuziteketeza kwa moto.
Hata hivyo Lupogo alipohojiwa alisema kwamba, agizo la Rais
John Magufuli “Hapa kazi tu” wamelipokea kwa mikono miwili na hivyo hawanabudi
kulifanyia utekelezaji, kama vile kuzingatia suala la usafi ili waweze
kuepukana na magonjwa mbalimbali.
No comments:
Post a Comment