Na Steven
Augustino,
Tunduru.
SERIKALI wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, imewataka Madiwani
wake kumaliza tofauti zao za kisiasa
ili waweze kuisaidia Halmashauri yao ya wilaya, kusukuma mbele maendeleo ya
wananchi waliowachagua.
Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa muda ambaye aliteuliwa kusimamia
shughuli za kuwaapisha madiwani hao, ambaye ni Katibu tawala wa wilaya ya Tunduru
Ghaib Lingo, wakati akifungua kikao hicho kilichofanyika kwenye ukumbi wa
Klasta ya walimu tarafa ya Mlingoti mjini hapa.
Lingo alisema endapo madiwani watashindwa kuvua makoti ya itikadi
za vyama vyao ambavyo viliwafanya kuingia madarakani, upo uwezekano mkubwa wa wilaya
hiyo kutopiga hatua mbele za kimaendeleo.
Huku wakiongozwa na Hakimu mfawidhi wa Mahakama ya wilaya hiyo,
Gladys Nancy Barthy katika kula viapo vyao vya udiwani madiwani wote
waliahidi kuwatumikia wananchi kwa moyo na nguvu zao zote, kwa kufuata kanuni
na miongozo iliyowekwa na serikali.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, nao wabunge wa majimbo ya
Tunduru Kusini Daimu Idd Mpakate, Tunduru Kaskazini Mhandisi Ramo Matala Makani
na Mbunge wa viti maalum Sikudhani Chikambo kwa pamoja waliwataka madiwani hao
kuunganisha nguvu zao, ili kufanikisha utekekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM) inayotekelezwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Mbunge wa viti maalum, Sikudhani Chikambo pamoja na kuwapongeza
madiwani hao aliwaomba kuimarisha umoja wao na kuachana na ushabiki wa vyama
ambao hautaweza kuwasaidia, katika kuwaletea maendeleo wananchi walio wachagua.
Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kusini, Daimu Mpakate alisema hivi
sasa wanayo kazi ngumu ya kutekeleza matakwa ya wananchi walio wachagua, hivyo inabidi
wajipange na kuhakikisha kwamba maendeleo yaliyotarajiwa yanafanikiwa kwa
wakati.
Mbunge wa jimbo la Tunduru Kaskazini, Mhandisi Ramo Makani
aliwataka kurejea na kufanya kwa vitendo utekelezaji wa maendeleo ya wananchi
na kwamba utekelezaji huo ulenge kushughulikia, kero zinazowakabili wananchi
wao.
No comments:
Post a Comment