Na Steven Augustino,
Tunduru.
ZUHURA Ngaharo ambaye anaishi katika kijiji cha Mkowela
wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, amevamiwa nyumbani kwake na watu wanaodaiwa
kuwa ni majambazi na kumpora fedha shilingi milioni 2.7 za mauzo ya duka lake.
Tukio hilo lilitokea majira ya usiku, Disemba 21 mwaka huu
baada ya majambazi hao kumteka na kumlazimisha kuwapatia fedha hizo za mauzo.
Diwani wa kata ya Nakapanya, Kubodola Ambali alisema kuwa
katika tukio hilo mama huyo ambaye ni mjane alivamiwa na watu wawili huku
wakiwa na silaha ya moto, bunduki na za jadi ambazo ni visu na mapanga
jambo ambalo lilimtisha maisha yake.
Alisema baada ya kumteka, watu hao walimwamuru kuingia dukani
na kuwapatia fedha hizo na asingefanya hivyo walikuwa wakimtishia kwamba wangepoteza
maisha yake, yeye na watoto ambao anaishi nao nyumbani hapo.
Baada ya maharamia hao kupata kiasi hicho cha fedha, waliondoka
na kutokomea kusikojulikana.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela amethibitisha
kuwepo kwa tukio hilo na kuongeza kuwa tayari amekwisha tuma kikosi cha askari
shupavu, kwa ajili ya kuwasaka watuhumiwa hao.
Aidha amewaomba wananchi, ambao wanaweza kuwa na taarifa
zozote juu ya watu ambao wamekuwa wakifanya uhalifu katika matukio tofauti
mkoani humo, kuwataja ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Endapo
wataendelea kuwaficha watu hao, ipo hatari ya kuendelea kupata madahara makubwa
yatakayosababishwa na wahalifu hao wanaowaficha, nawataka wananchi waendelee
kujenga ushirikiano kwa kuwataja popote pale walipo ili tuweze kuwakamata na
kuwafikisha kwenye vyombo vya kisheria”, alisema.
No comments:
Post a Comment