Na Steven Augustino,
Tunduru.
MAELFU ya Wananchi katika wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma,
wamepongeza maamuzi ya serikali ya awamu ya tano, kufanya maadhimisho ya sherehe
za miaka 54 ya Uhuru kwa kufanya usafi, jambo ambalo Watanzania linawakumbusha
kuwa ni wamoja.
Hayo yalibainishwa na wananchi hao kwa nyakati tofauti,
walipokuwa wakizungumza na mwandishi wetu wakati walipokuwa wakishiriki katika zoezi
la kufanya usafi kwenye maeneo yao, kwa lengo la kuweka mazingira yao katika
hali ya usafi ili kuweza kupambana na adui maradhi.
Miongoni mwa waliopata nafasi ya kuzungumzia tukio hilo, ni
pamoja na mtendaji wa kata ya Nakayaya wilayani humo, Zainabu Issa
ambaye alikutwa akiwa na timu yake wakifanya usafi katika eneo la kata hiyo.
Alisema kuwa awali wananchi wengi walijenga dhana kwamba,
jambo la usafi katika maeneo ya mijini au masoko ni jukumu la serikali pekee
lakini baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli kuonesha
njia kila mtu ameanza kutambua kuwa usafi ni wajibu wa kila mtu.
Wengine ni fundi mkuu wa mitambo katika viwanda vya kubangulia
korosho wilaya ya Tunduru, Masasi, Newala na Mtwara Mhandisi Sivan Edayeth
ambaye alisema kwamba usafi wa mazingira katika maeneo tunayoishi ni jukumu la
kila mtu ili kuweza kuepukana na wadudu ambao huleta magonjwa mbalimbali.
Mkuu wa wilaya ya Tunduru, Agnes Hokororo ambaye aliwaongoza
mamia ya watumishi wa idara ya serikali katika zoezi hilo kwenye maeneo ya
ofisi za Boma, Halmashauri, Hospitali ya Wilaya na kuhitimisha shughuli hiyo
katika eneo la soko kuu la Azimio alisema usafi wa mazingira katika maeneo yao
yatakuwa endelevu.
Naye Mkurugenzi mtendaji wa Hamashauri ya wilaya ya Tunduru,
Tina Sekambo alisema kuanzia sasa hakuna mtu, atakaye vumiliwa endapo atapuuzia
agizo la kufanya usafi katika eneo lake.
No comments:
Post a Comment