VILIO na simanzi vimetawala
baada ya wakazi waishio katika eneo la Jangwani jijini Dar es Salaam, kukumbwa
na bomoa bomoa ambapo nyumba zaidi ya 100 zimebomolewa katika siku ya kwanza
katika eneo la Mkwajuni na Magomeni katika Manispaa ya Kinondoni.
Jana Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Baraza
la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Manispaa za Jiji la Dar es Salaam,
zilianza kazi ya kubomoa nyumba zote zilizo katika maeneo oevu, kando ya mito
na bahari.
Mkuu wa Kitengo cha Sheria Baraza la Taifa la Usimamizi wa
Mazingira Tanzania (NEMC), Manchale Heche alisema bomoa bomoa hiyo inalenga
kuzibomoa nyumba zaidi ya 4,000 zilizojengwa katika maeneo hayo huku nyingi
zikiwa ni katika bonde la mto Msimbazi.
“Leo hapa Jangwani tumeanza kwa kubomoa nyumba zaidi ya 100,
lakini nyumba zaidi ya 4,000 zinatarajiwa kubomolewa na hizi ni zile zote
ambazo zimejengwa katika maeneo ambayo yanakatazwa kisheria,” alisema Heche.
Heche alisema serikali ilishatoa tangazo la mwisho juu ya
kuwataka wakazi wote waliojenga katika maeneo ya mabondeni, na maeneo yote hatarishi
wahame, lakini watu wameendelea kukaidi.
“Tumekuwa tukiwasihi kuhama maeneo ya mabondeni kila mara,
Serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete, ilishawatangazia
wananchi wa mabondeni wahame na aliwapa viwanja huko Mabwepande, lakini wameviuza
na kuendelea kujenga na kuishi mabondeni kinyume cha sheria za mazingira na
mipango miji,” alifafanua Mwanasheria Heche.
Nyumba zitakazokumbwa na bomoa bomoa hiyo ni zile
zilizojengwa maeneo yote ya bondeni katika bonde la mto Msimbazi, kando ya mito
na katika maeneo ya hifadhi ya bahari ndani ya mita 60.
Aidha, Mwanasheria huyo alisema bomoa bomoa hiyo ni endelevu,
hivyo kuwataka wananchi wote wanaoishi maeneo ya miundombinu na maeneo yote
hatarishi, iki wemo katika fukwe za bahari, kingo za mito na mikondo ya bahari
kuhamisha mali zao mapema kabla hawajafikiwa.
Wakazi wote waliopo katika bonde la mto Msimbazi, ikiwa ni
kuanzia Jangwani hadi maeneo ya Gongo la Mboto, katika Manispaa ya Kinondoni na
kwingineko, wanapaswa kuhama.
Wakazi waliokutwa na kadhia hiyo, kwa nyakati tofauti
wamesikika wakilalamika kutokuwa na taarifa japo mara kadhaa Rais mstaafu
Jakaya Kikwete, aliwatangazia kuhama kwa hiyari.
Heche alisema ubomoaji huo haulengi Dar es Salaam pekee, bali
ni kazi inayofanyika nchi nzima na wote waliojenga mabondeni na katika maeneo
oevu, wahame.
Alisema wao wanalenga kulinda usalama wa wananchi kimazingira
na kiafya, kwa ujumla kwa maeneo hayo ni hatari na wenyewe ni mashuhuda pindi
patokeapo mvua wanakumbwa na mafuriko.
Mwezi uliopita, Manispaa ya Kinondoni iliendesha bomoa bomoa
kwa watu waliojenga katika maeneo ya wazi na ilieleza kuwa kazi hiyo itakuwa
endelevu.
No comments:
Post a Comment