Na Bashir Yakub,
SOTE tunajua kwamba kila atendaye
kosa sharti aadhibiwe. Na kuadhibiwa huko lazima
kuwe kwa mujibu wa sheria, pamoja na
kuwa mtenda kosa hustahili adhabu bado watenda kosa hutofautiana
hadhi. Hadhi hapa sio kuwa fulani
ni mkuu wa mkoa au mkurugenzi
na fulani ni mkulima wa kawaida kijijini
Katanakya.
Hadhi ndio kama hizo zilizotajwa
katika kichwa cha makala. Wapo watenda
makosa lakini wakiwa na umri mdogo,
wapo watenda makosa lakini wakiwa hawana
akili timamu halikadhalika wapo watenda
makosa lakini wakiwa na akili isiyo ya kawaida
kwa maana ya akili ya ulevi.
Sheria inasemaje juu ya hawa wote
kuanzia utendaji wao wa makosa, kushitakiwa
na kuwajibika kwao. Makala haya yataeleza
ili tujue hadhi ya kimashitaka ya
makundi haya.
1.JE MWENYE
UGONJWA WA AKILI ANAWEZA KUSHITAKIWA ?
Jibu ni ndiyo sheria haikatazi
kumshitaki mwenye ugonjwa wa akili (chizi). Kuna
tofauti kati ya kushitakiwa na kuwajibika, kushitakiwa
ni kumfungulia mashtaka na kuwajibika ni
kupata adhabu baada ya kupatikana na hatia. Hivyo
kushitakiwa atashitakiwa, isipokuwa sheria inatoa
mwongozo kuhusu kuwajibika kwake.
Kifungu cha 13 ( 1 ) cha Kanuni
za adhabu sura ya 16 kinasema kuwa mtu
hatawajibika kwa kutenda kosa la jinai,
iwapo wakati wa kutenda kitendo hicho
alikuwa katika hali ya ugonjwa wowote unaoathiri
akili yake. Hiyo ni kanuni ya jumla
iliyowekwa na kifungu hicho.
Hata hivyo kifungu hicho hicho
kimeweka masharti kuwa yapo mazingira
ambayo mwenye ugonjwa wa akili atatakiwa
kuwajibika. Kinasema kwamba mwenye ugonjwa wa
akili hatawajibika kwa kutenda kosa la
jinai iwapo tu wakati anatenda kosa
alikuwa hajui anachokitenda, hana uwezo
wa kutambua kuwa hapaswi kutenda kosa
na hana uwezo wa kuzuia kitendo hicho.
Hii maana yake kwamba, ikiwa
mgonjwa wa akili anao uwezo wa kujitambua
wakati akitenda kosa basi atapatikana na
jinai hata kama ameua kwa makusudi
atahukumiwa kunyongwa.
Maswali ya kitaalamu (Examination)
atakayoulizwa Mahakamani ndiyo yatakayotoa majibu
ikiwa alikuwa anajitambua wakati wa kutenda
kosa au la. Hii ni kwasababu akademia
ya tiba inaonesha kuwa machizi
wengi si wakati wote huwa hawajitambui.
Upo wakati huwa wanajitambua na
upo wakati hawajitambui. Kutokana na hili
isingekuwa sahihi kuwaacha watende walitakalo
muda wote kwa kinga ya ugonjwa wa akili, kama
hili lingeachwa kungekuwa pia na uwezekano
mkubwa kwa wenye akili timamu kutumia
nafasi hiyo, kutenda jinai huku wakitegemea
kinga ya utimamu wa akili.
2. JE ULEVI
NI KINGA BAADA YA KUTENDA KOSA ?
Kifungu cha 14(1) cha kanuni za
adhabu kinasema kuwa kulewa hakutachukuliwa
kama kinga dhidi ya kosa lolote la jinai.
Hii ni kanuni ya jumla. Yumkini yapo
mazingira ambapo ulevi unaweza kuwa
kinga baada ya kutenda jinai.
Tunaposema kinga tunamaanisha kuwa,
mtu atashitakiwa lakini atajitetea kuwa
nilikuwa nimelewa au sina akili timamu na
kutokana na utetezi huo atatakiwa kuachiwa
huru, hii ndio maana ya kinga.
3. MAZINGIRA
AMBAYO ULEVI NI KINGA BAADA YA
KUTENDA KOSA.
Ili kulewa iwe kinga baada
ya kutenda jinai sharti la kwanza ni
kuwa wakati mlevi anatenda kosa, iwe
kweli ulevi ule ulimfanya awe hajitambui
kiasi cha kutojua anachotenda.
Pili ulevi ule usiwe
umepatikana kwa hiari yake, na hili ndiyo jambo
la msingi sana. Ukienda mwenyewe kilabuni au
nyumbani kwako ukanywa ukalewa ukawa
hujitambui na hatimaye kutenda jinai, ulevi haitakuwa
kinga kwako abadani, ili iwe kinga ni
lazima iwe haukulewa kwa hiari yako.
Hapa ina maana kuwa
ulilazimishwa kulewa au ulileweshwa sasa kuleweshwa au kulazimishwa
kulewa hapa sio kununuliwa pombe
ukanywa, hapana !
Kuleweshwa au kulazimishwa kulewa
ni kwa mfano, umechanganyiwa pombe kwenye
kinywaji kingine bila wewe kujua au
umewekewa dawa za kulevya kwenye chakula,
kinywaji bila wewe kujua. Hapa ndipo ulevi
unaweza kusimama kama kinga na hivyo
kuondokana na hatia ya jinai.
Mazingira mengine ulevi
unaweza kuwa kinga hasa pale mwenye ugonjwa
wa akili na kutokana na ugonjwa huo,
atajilewesha mwenyewe na kutokana na kulewa
huko akatenda jinai.
Ulevi utakuwa kinga kwake kwa kuwa
uchizi, ndio ulimsababishia alewe na
hivyo haikuwa katika hiari ya kawaida, kwa
ujumla niseme tu hivi ndivyo ilivyo kwa
hili la ulevi na kutokuwa na akili
timamu.
No comments:
Post a Comment