DAR ES SALAAM.
RAIS Dokta John Magufuli amekutana na kuzungumza na aliyekuwa
mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif
Hamad juu ya mgogoro wa uchaguzi mkuu, wa Rais wa visiwa hivyo
unaoendelea kufukuta chini chini.
Mkutano huo baina ya viongozi hao, umefanyika ikiwa ni siku
kadhaa tangu Bodi ya MCC kutangaza kusitisha msaada wa dola Milioni 472.8 ambazo
ni sawa na takribani Sh trillioni moja, kwa sababu ya mgogoro huo.
Fedha hizo zililenga kusaidia sekta ya nishati ya umeme,
hususan ule wa vijijini kwa kuunganisha wateja wapya na kufanya mabadiliko ya
kimuundo ya Shirika la ugavi wa Umeme (TANESCO) ili lifanye kazi na kutoa
huduma, kwa ufanisi zaidi katika sehemu za uzalishaji, usafirishaji na
usambazaji.
Fedha hizo pia zilikusudiwa kusaidia kuanza kwa mpango mkubwa,
wa kuboresha sekta ya umeme nchini 2014-2024.
Mazungumzo ya viongozi hao wawili yamehudhuriwa pia na Makamu
wa Rais, Samia Suluhu Hassan.
Viongozi hao kwa pamoja wamejadili hali ya kisiasa Zanzibar,
na wamaefurahishwa na hali ya usalama na utulivu inayoendelea.
Rais Dokta Magufuli ameamuahidi Maalim Seif kwamba, mazungumzo
yataendelea hadi suluhisho la kisiasa litakapopatikana.
No comments:
Post a Comment