Na Mwandishi wetu,
Songea.
WATENDAJI wa vijiji na kata wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, wameagizwa
kuwakamata na kuwachukulia hatua kali watu wote wanaojihusisha na uchafuzi wa
mazingira na uharibifu wa vyanzo vya maji katika maeneo yao.
Agizo hilo limetolewa hivi karibuni na Mkurugenzi mtendaji wa
Halmashauri ya wilaya hiyo, Sigsbert Kaijage wakati alipokuwa akifunga kikao
cha siku moja cha Wadau wa zao la muhogo, kilichoandaliwa na Muunganisho wa
Vikundi vya Ujasiriamali Vijijini (MUVI) kwenye ukumbi wa Chuo kikuu huria uliopo
mjini hapa.
Kadhalika ameagiza kutumia sheria ndogo za Halmashauri, ili
kuweza kuwabana na kuwafikisha Mahakamani watu wanaojihusisha na uchomaji
misitu hovyo ambao wamesababisha baadhi ya maeneo mkoani humo, kuanza kugeuka
jangwa na kupungua kwa kiwango cha mvua.
“Watu wanaochoma moto na uharibifu wa mazingira katika maeneo
yetu tunawatambua, tutumie sheria zilizopo kuwafikisha Mahakamani kwani tayari
athari zimeanza kuonekana juu ya uharibifu huu ambao unaendelea kufanyika”, alisema
Kaijage.
Alisema kuwa hali ya mazingira katika maeneo mengi
ya mkoa wa Ruvuma, yameharibiwa kutokana na kasi kubwa ya uchomaji moto
misitu jambo ambalo linatishia mkoa huo, kuanza kugeuka kuwa jangwa na kupotea
kwa vyanzo asili vya maji na wanyama ambao wanatumika kwa ajili ya utalii wa
ndani.
Watumishi wa serikali amewataka kutambua kwamba, wao ndiyo
jicho la wananchi hivyo ni vyema wawe mfano bora na wakuigwa kwa kuendelea
kuelimisha jamii, juu ya kuachana na vitendo vya uharibifu huo wa mazingira.
No comments:
Post a Comment