WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ametoa siku mbili kwa Katibu Tawala wa
Mkoa wa Kigoma, Eng. John Ndunguru kukamilisha uchunguzi wake na kumpatia
taarifa ya maandishi juu ya tuhuma ubadhirifu wa fedha za umma unaohusisha
uuzwaji wa jengo la KIGODECO na viwanja 12 vya Manispaa ya Kigoma/Ujiji ambao
unadaiwa kukiuka taratibu.
Ametoa agizo hilo leo mchana (Jumatano, Desemba 30, 2015) kwenye
ukumbi wa NSSF, mjini Kigoma wakati akizungumza na viongozi na watendaji
mbalimbali wa mkoa huo alipokuwa akifanya majumuisho ya ziara yake ya siku
mbili mkonai humo.
Waziri Mkuu Majaliwa amesema anazo taarifa kuwa jengo hilo
liliuzwa kwa sh. milioni 370/- pamoja na jengo jingine la MIBOS kwa sh. milioni
50/- licha ya kupewa barua na Mkuu wa Mkoa huo kusitisha uuzwaji wa jengo
pamoja viwanja hivyo, bado liliuzwa.
“Katibu Tawala wa Mkoa kaa na Mkurugenzi wa Manispaa,
Mhandisi wa Manispaa na Mhasibu na unipatie taarifa kwa maandishi ifikapo
Jumamosi hii,” alisema Waziri Mkuu huku akishangiliwa.
“Nataka kujua nani alifanya tathmini ya jengo, ni kwa nini
jengo liliuzwa kwa thamani hiyo, je ndiyo thamani halisi ya jengo? Ni kwa nini
RC alipozuia, utaratibu uliendelea? Je, utaratibu wa uuzaji ulifuatwa? Ni kwa
nini viwanja viliuzwa chini ya thamani,? Katibu Tawala kaa na watu wako na
uniletee hiyo taarifa kwa maandishi. Tukigundua kuna mianyamianya tutachukua
hatua za kinidhamu,” alisema.
Viongozi walioagizwa kukutana na Katibu Tawala wa Mkoa ni
Mkurugenzi wa Manispaa, Eng. Boniface Nyambele; Mhandisi wa Manispaa, Eng.
Boniface William na Mhasibu wa Mapato wa Manispaa, Ndg. Bawili Mkoko.
Kuhusu uuzwaji wa jengo na viwanja, imebainika kuwa Mkuu wa
Mkoa huo, Luteni Kanali (Mst), Issa Machibya alizuia uuzaji huo kwa barua ya
tarehe 16 Juni 2015 akitaka viwanja hivyo vitumike kwa matumizi ya manispaa na
mchakato huo usitishwe hadi mwakani lakini agizo lake lilipuuzwa na jengo
likauzwa kwa sh. milioni 370 ambayo ni bei ya kiwanja pekee.
Tuhuma nyingine zinazopaswa kuchunguzwa ni pamoja na
matumizi ya sh. milioni 809 kwa ajili ya ujenzi wa maabara. Kiasi hicho
kilitolewa kutoka kwenye fedha za miradi ya maendeleo (Capital Development
Grants-CDG), Mradi wa Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo na Mifugo (ASDP),
Mradi wa Uendelezaji Miji (Tanzania Strategic Cities Programme –TSCP) na Miradi
ya Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (SEDP).
Inadaiwa kwamba Mkurugenzi huyo kwa kushirikiana na baadhi
ya watumishi wa idara ya mipango na fedha walitumia ujenzi wa maabara kama
kigezo cha kuchota fedha hizo bila kutoa taarifa kwa wakuu wa idara husika
ambao walikasimiwa fedha hizo.
Tuhuma nyingine ni manunuzi hewa ya vipuri (spare parts)
vyenye thamani ya sh. milioni 8 na manunuzi hewa ya stationeries yenye thamani
ya sh. milioni 4.6/-. Haya yanadaiwa kufanywa Julai 25, mwaka huu na Mkurugenzi
huyo akishirikiana na Mhasibu Mkoko.
Waziri Mkuu amerejea jijini Dar es Salaam mchana huu.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, DESEMBA 30, 2015.
No comments:
Post a Comment