Na Kassian Nyandindi,
Songea.
MBUNGE wa Jimbo la Songea mjini, Leonidas Gama amewataka
vijana waliopo katika jimbo hilo kuunga mkono jitihada mbalimbali
zinazofanywa na Rais Dokta John Magufuli, juu ya namna anavyowashughulikia baadhi
ya watendaji wabovu waliopo Serikalini ikiwa ni lengo la kuongeza kasi ya
uwajibikaji kazi, katika maeneo yao ili Taifa liweze kukua kimaendeleo.
Gama alisema hayo juzi mjini Songea, alipokuwa akizungumza na
waendesha pikipiki maarufu kwa jina la boda boda mara baada ya kumaliza kazi ya
kufanya usafi, katika kata ya Ruhuwiko mjini hapa.
Alisema kuwa Watanzania wote wanakubali kwamba wamepata Rais
bora, hivyo ni njia pekee sasa ya kuendelea kumuunga mkono ili aweze kukomesha
vitendo vya rushwa, wizi na ufisadi vinavyofanywa na baadhi ya watumishi wa
umma ambao sio waaminifu.
Vilevile alisema kuwa hatua hiyo itasaidia kuharakisha
ukuaji wa uchumi kwa mtu mmoja mmoja, wilaya na taifa kwa ujumla kwa kile
alichoeleza kuwa hivi sasa hata miradi ya maendeleo utekelezaji wake, utalingana
na gharama halisi ya fedha zinazotolewa na serikali.
Alifafanua kuwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM)
inatambua mchango mkubwa wa vijana wanaojishughulisha na biashara ya boda boda,
ndiyo maana iliamua kuvunja sheria inayokataza chombo cha magurudumu mawili
kubeba abiria ili vijana wengi wasiokuwa na kazi, wapate fursa ya kujiajiri
kupitia boda boda na waweze kuwa na kipato.
Kupitia vikao vya Halmashauri ya Manispaa ya Songea, alisema
atahakikisha wanafuta ushuru mdogo mdogo ambao ni kero kubwa kwa wafanyabiashara
hasa akina mama wauza matunda na mboga mboga, kwani kero hiyo endapo itaachwa
kwa muda mrefu huchangia kuwarudisha nyuma kiuchumi.
Mbali na hilo Gama alifafanua kuwa Madiwani wote wa Manispaa
hiyo, bila kujali itikadi za vyama vyao wamekubaliana juu ya suala la kuinua
uchumi wa mji huo kwa kuhimiza wananchi kutumia muda mwingi kufanya kazi za
uzalishaji mali, kusimamia mapato na kudhibiti matumizi mabaya ya fedha
zinazokusanywa kutoka katika vyanzo mbalimbali.
Aidha ameahidi kwamba, atahakikisha anasimamia kikamilifu mikopo
kwa vijana na wanawake ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri ili waweze
kujiinua kiuchumi, badala ya kuendelea kuwa tegemezi kwa watu wengine.
Hata hivyo amewaasa waendesha boda boda hao, kufuata sheria
za usalama barabarani ikiwemo kuvaa kofia ngumu na kubeba abiria mmoja, kuacha
kubeba wahalifu na kulisaidia Jeshi la Polisi kuwafichua watu wanaojihusisha
na vitendo hivyo kama vile ukabaji, wizi wa kutumia silaha na hata
wasichana wanaofanya biashara haramu ya ngono.
No comments:
Post a Comment