Na Mwandishi wetu,
Songea.
HALMASHAURI ya wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma, imekamilisha
mradi wa upimaji viwanja 500 katika kijiji cha Madaba wilayani humo,
ambavyo vitatumika kwa ajili ya ujenzi wa mji mpya wa wilaya hiyo.
Upangaji mpya wa eneo hilo, umeanza na
upimaji viwanja katika maeneo ambayo wananchi wanayatumia kama mashamba
ambapo wametakiwa kuyaachia ili kupisha kazi hiyo, hatua inayotajwa kwamba
itaweza kubadili sura ya wilaya hiyo mpya na kuwa mji mdogo.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi mtendaji wa Halmshauri
hiyo, Robert Mageni alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari na kueleza
kuwa upangaji mpya wa eneo la kijiji cha Madaba na maeneo jirani,
utazingatia ramani itakayochorwa na wataalamu husika kutoka idara ya ardhi.
Alisema kuwa kutokana na uboreshaji wa eneo
hilo, baadhi ya maeneo yatachukuliwa na serikali kwa ajili ya ujenzi wa huduma
mbalimbali za kijamii ikiwemo huduma za afya, kituo cha Polisi na mabasi
likiwemo pia soko la kisasa na kwamba wananchi wanaomiliki maeneo hayo watalipwa
fidia.
Kwa mujibu wa Mageni alieleza kuwa kutokana na
hatua hiyo, viwanja vingine vitauzwa kwa watu binafsi, taasisi za serikali na
mashirika ya dini ambapo tayari Kanisa katoliki Jimbo la Njombe limeonesha
kuhitaji maeneo, kwa ajili ya ujenzi wa vitega uchumi katika kijiji
hicho.
Alisema kuwa watu na taasisi zitakazopewa viwanja hivyo,
watatakiwa kujenga nyumba za kisasa na kufanya uwekezaji wa aina mbalimbali,
ikiwa ni lengo la kufanya Madaba uwe mji mzuri wa kibiashara.
“Tunatambua umuhimu wa shughuli za kilimo
zinazofanywa na wananchi wetu katika eneo hili, hata hivyo tunawaomba wananchi
watusamehe kutokana na usumbufu utakaojitokeza kwani kila
kitakachotekelezwa ni kwa manufaa ya watu wote”, alisema Mageni.
Aliongeza kuwa, uboreshaji huo utawezesha
wananchi kupata huduma muhimu kwa urahisi kama vile maji safi
na salama, miundombinu ya barabara, umeme wa uhakika ambao utaunganishwa na
gridi ya Taifa unaoendelea kujengwa kutoka Makambako hadi Songea kupitia wilaya
hiyo ya Madaba.
No comments:
Post a Comment