Na Steven Augustino,
Tunduru.
BAADHI ya wananchi wa kijiji cha Nakayaya wilaya ya Tunduru
mkoani Ruvuma, wamegoma kupokea fidia zao walizotakiwa kulipwa na Halmashauri
ya wilaya hiyo, ikiwa ni malipo ya fidia ya ardhi na mashamba yakiwemo na
majumba wanayoishi ambayo yalipimwa na kuwataka wahame.
Mgomo huo wameufanya takribani miaka mitatu sasa, ambapo
maeneo hayo yalipimwa kwa lengo la kuweka makazi kwa mfumo wa ramani ya mipango
miji ya wilaya hiyo.
Kufuatia hali hiyo wananchi hao, wamemuomba Waziri wa ardhi
nyumba na maendeleo ya makazi, William Lukuvi kuingilia kati na kuwasaidia
kupata haki zao za msingi zinazoonekana kutaka kuporwa na viongozi hao wa
Halmashauri, wanaotumia mbinu za ujanja ili kutaka kupora haki za wananchi hao kwa
lengo la kujinufaisha wenyewe baada ya kupima, kuyagawa kwa watu wengine na
kuwatimua katika maeneo yao.
Wananachi hao walisema wamelazimika kupeleka maombi hayo kwa
Waziri Lukuvi, kutokana na wao kuwa na matumaini ya utendaji wake na
kwamba endapo atachelewa kuchukua hatua, ipo hatari ya kuzuka kwa mapigano kati
yao na watu waliouziwa maeneo hayo na halmashauri hiyo, kwani hivi sasa wamekuwa
wakifanya uhalifu mkubwa wa kukata mazao yao ya kudumu waliyopanda ikiwemo miti
ya matunda, iliyopo katika maeneo hayo.
Wakifafanua juu ya hali hiyo kwa nyakati tofauti, walisema kilichowasukuma
kuchukua maamuzi hayo kinatokana na kubaini uwepo wa mchezo mchafu
ulioambatana na vitendo vya uchakachuaji wa haki zao, uliopangwa kutekelezwa na
viongozi wa Halmashauri yao.
Mmoja kati ya wasemaji wa wahanga hao, Jafary Muhyela alisema
kuwa miongoni mwa vitu vilivyowafanya wasipokee cheki za malipo yao, ni kitendo
cha usiri uliowekwa katika utaratibu wa malipo hayo ambayo hayaelezi uwazi na
taratibu zilizotumika juu ya viwango halisi vya malipo.
Alisema hundi hizo ambazo ziliandikwa mwezi wa nne mwaka
2013, pamoja na kuonesha majina ya walengwa wa malipo hayo lakini hundi
hazikuonesha kiasi cha fedha walizostahili kupokea na badala yake, walitakiwa
kupokea hundi hizo zikiwa ndani ya bahasha zimefungwa huku kukiwa na maelekezo
ya kuwataka wakazifungulie benki, wakiwa hawajui kiasi halisi cha fedha walichopokea.
Wananchi wengine waliogoma kupokea hundi hizo ni Longinus Rihard,
Fatuma Mlanda, Laika Hamis, Daud Gwasa na Rashid Gwasa.
Kadhalika wengine ni Zainabu Gwasa, Rihard Ngonyani, Cosmas
Mwimba, Mohamed Gwasa, Rukia Isaa, Magreth Mhyela na Jafary Muhyela ambaye
alitakiwa kupokea miongoni mwa hundi hizo na kwamba hata wakati tathimini ya
fidia zao ilipofanyika, wao hawakupatiwa hata nakala ya kumbukumbu za mali zao.
Alisema wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo hawakushirikishwa
kikamilifu, jambo ambalo ni ukiukwaji wa
sheria ya ulipaji wa fidia ya ardhi inayoelekeza kwamba baada ya kufanyika kwa
tathimini, wahusika walipwe ndani ya miezi sita.
Jambo jingine lililowashangaza ni kitendo cha viongozi
wa Halmashauri ya wilaya ya Tunduru, kuwanyima wamiliki wa mashamba hayo hata
kipande cha kujenga katika ardhi wanayoimiliki kimila kwa muda mrefu, ambapo
taarifa zinaeleza kuwa wazee hao walikimbilia katika maeneo hayo wakati wa vita
vya Majimaji jambo wanalolitafsiri kuwa kitendo hicho ni ukiukwaji wa taratibu
za haki za binadamu.
Walipotakiwa kuzungumzia mkanganyiko huo, Ofisa ardhi na
maliasli wa wilaya hiyo, Japhet Mnyagala na wa mipango miji mji wa Tunduru,
Naon Chalale walikataa kuzungumzia juu ya malalamiko hayo wakisema kwamba wao
siyo wasemaji juu ya suala hilo.
Akizungumzia tukio hilo, Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri
ya wilaya hiyo Tina Sekambo alikiri kuwepo kwa mgogoro huo na kuongeza kuwa
kilichofanywa na uongozi huo ni halali, kwani taratibu haziruhusu kuwekwa wazi
siri za mtu yeyote.
"Kilichofanywa na wataalamu wangu kipo sahihi, kwani
taratibu na miongozo ya ulipaji wa fedha haziruhusu kuwekwa wazi kwa kila mtu”,
alisema Sekambo na kuongeza kuwa kutokana na kusuasua kwao kupokea malipo hayo
tayari cheki zao zimekwisha muda wake (zimechacha) Oktoba 27/2013.
Sekambo aliendelea kufafanua kuwa wananchi hao wangepokea malipo
hayo na baada ya kutafakari juu ya mapunjo wanayozungumzia, wangeandika barua
za malalamiko ya kuomba kuongezewa malipo.
Alisema kwa sasa Halmashauri yake haijui itawasaidiaje na
akawashauri kwenda kuishitaki katika baraza la ardhi, ili waweze kufikia muafaka
juu ya mgogoro huo.
No comments:
Post a Comment