Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga vijijini mkoani
Ruvuma, wametakiwa kujenga ushirikiano katika kusimamia na kukagua miradi ya
maendeleo ya wananchi, ili iendane na thamani halisi ya fedha zinazotolewa na
serikali.
Aidha imeelezwa kuwa kutokana na baadhi ya Madiwani na
watendaji wa serikali kutosimamia ipasavyo miradi hiyo, wamekuwa wakisababisha
miradi mingi kutoendana na thamani halisi ya fedha iliyotolewa.
Madiwani wapya wa Halmashauri ya wilaya Mbinga vijijini wakila kiapo. |
Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Senyi Ngaga alisema hayo wakati
alipokuwa akiwasilisha salamu za serikali kwenye kikao cha baraza la Madiwani Halmashauri
ya Mbinga vijijini, kilichoketi kwenye ukumbi wa Umati uliopo mjini hapa.
“Ndugu zangu, wenyewe mnaona kasi ya ufanyaji kazi kwa
serikali hii ya awamu ya tano, watumikieni wananchi ipasavyo ili tuweze
kuwaletea maendeleo mambo ya uchaguzi yamepita tuondoe tofauti zetu, sasa
tunaingia katika utekelezaji kwa kufanya kazi za serikali”, alisema Ngaga.
Ngaga alieleza kuwa matarajio ni kuona madiwani na watendaji
wake wa serikali, wanatimiza majukumu ya wananchi ipasavyo ili kuondoa
malalamiko yasiyokuwa ya lazima, ambayo baadaye husababisha migogoro miongoni
mwa jamii.
Pamoja na mambo mengine, katika kikao hicho cha baraza la
madiwani waliweza kufanya uchaguzi wa kumchagua Mwenyekiti wao, atakayeweza
kuongoza baraza hilo kwa kipindi cha miaka mitano.
Ambrose Nchimbi ambaye ni diwani wa kata ya Amani makolo,
kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliweza kushinda katika nafasi hiyo
kwa kupata kura 37 huku akimbwaga chini mpinzani wake wa Chama Cha Demokrasia
na Maendeleo (CHADEMA), Edmund Nditi aliyepata kura 1.
Hata hivyo kwa nafasi ya makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya
wilaya ya Mbinga vijijini, ilichukuliwa na Benuard Komba wa CCM ambaye alipita
bila kupingwa.
No comments:
Post a Comment