Na Julius Konala,
Songea.
ZAIDI ya watoto 300 wamebatizwa Jumapili ya sherehe za krismasi
kwenye Kanisa katoliki Parokia ya Bombambili, Jimbo kuu la Songea mkoani Ruvuma
kitendo ambacho kimeelezwa kuwa ni cha kihistoria kwa madai kwamba, ni mara ya
kwanza kutokea tangu kuanzishwa kwa Parokia hiyo.
Ibada hiyo ya misa takatifu ya ubatizo iliongozwa na Padri
Godfrey Nchimbi, huku akisaidiwa na mapadre wengine mbalimbali wakiwemo Otieno
Olwen na Simon Ndunguru ambaye ni Paroko wa parokia hiyo ya Bombambili.
Sambamba na hilo jumla ya watu 73 walipata sakramenti ya ndoa
katika kanisa hilo, tukio ambalo lilitanguliwa na baadhi yao ambao hawakuweza
kufuata hatua za sakramenti kwa kufuata utaratibu wa kanisa, walianza kupewa
sakramenti ya ubatizo, kipaimara na kisha kufungishwa ndoa.
Matukio hayo yote mawili yalikwenda sambamba na kula chakula
cha pamoja kilichoandaliwa na Paroko wa parokia hiyo, Padri Simon Ndunguru
katika ukumbi wa mikutano wa parokia hiyo na kuhudhuriwa na waumini mbalimbali,
wakiwemo wasimamizi wa watoto wa ubatizo na ndoa.
Awali akihubiri katika ibada hiyo ya misa takatifu ya ubatizo
na ndoa, Padri Otieno Olwen amewataka wazazi kuwalea watoto wao katika misingi
ya maadili mema ili kanisa na taifa kwa ujumla, liweze kupata viongozi waadilifu.
Olwen alisema kuwa ufisadi, wizi na vitendo vingine viovu ni
matokeo ya wazazi kushindwa kuwalea watoto wao katika misingi ya uadilifu
ambapo amewataka wazazi na walezi wa watoto hao, kuhakikisha wanawafundisha
kufuata imani ya dini yao kwa kuhudhuria na kushiriki ibada mbalimbali.
Akizungumzia kwa upande wa wanandoa aliwataka kudumisha na
kuheshimu ndoa zao, badala ya kusikiliza maneno ya watu wa nje ambao wanaongea
uongo na kuchonganisha kwa malengo ya kuzifarakanisha huku akiwaasa
kuheshimiana na kuombana msamaha pindi wanapokorofishana.
No comments:
Post a Comment