Na Steven Augustino,
Tunduru.
WANANCHI waishio katika kijiji cha Tuwemacho kata ya
Tuwemacho wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wameipongeza serikali kwa uamuzi wa
kuwajengea zahanati kijijini humo ambayo wanaimani kwamba itawakomboa na adha
waliyoipata kwa muda mrefu sasa, juu ya upatikanaji wa matibabu ya uhakika.
Mwenyekiti kijiji hicho, Sijaona Ally Pekani alibainisha hayo
alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu ambaye alitembelea katika eneo hilo,
kujionea ujenzi huo ambao unaendelea.
Pekani alifafanua kuwa kutokana na wananchi wake, kukabiliwa
na kero hiyo kwa muda mrefu zaidi ya wananchi 2,000 kati ya wananchi wote 2,871
ambao wanaishi kijijini humo, wamejitokeza na kujitolea kuchangia nguvu zao juu
ya ujenzi wa mradi huo wa zahanati.
Mtendaji wa kata ya Tuwemacho, Ipyana John alisema ujenzi wa
mradi huo utasaidia kuwakomboa hata wananchi wanaoishi jirani kutoka vijiji vya
Nasya, Tuwemacho, Chemchem na Namasalau ambavyo wakati wote hutegemea kupata
huduma za matibabu katika Hospitali ya wilaya ya Tunduru ambayo ipo mbali nao.
Nao Mwenyekiti wa kamati ya ujenzi wa mradi huo, Swalehe Ally
Gemti na mjumbe wa kamati hiyo, Maua Yahaya walisema kwamba kukamilika kwa
ujenzi wa mradi huo utakuwa ni msaada mkubwa kwa wananchi hao na kuwaondolea
kero ya kutembea kwa miguu umbali wa zaidi ya kilometa 10, kufuata huduma
za matibabu ambazo hupatikana Tunduru mjini.
Walisema toka kijiji hicho kianzishwe mwaka 1974 hadi leo hii,
wananchi wamekuwa wakifuata huduma ya matibabu hospitali ya wilaya hiyo jambo
ambalo limekuwa likisababisha baadhi ya wagonjwa kupoteza maisha, wakati wakiwa
njiani kuelekea huko huku wakihatarisha pia usalama wa maisha yao kutokana na
wanyama wakali waliopo katika misitu iliyopo katika njia za kuelekea mjini.
Mradi huo unajengwa kwa ufadhili wa Mfuko wa Maendeleo
ya Jamii (TASAF) hapa nchini, tofauti na awali ulikuwa unajengwa chini ya mfuko
wa jimbo ambapo ulikwama kutokana na kukosekana fedha.
Akizungumza na mafundi wanaoendelea na kazi ya ujenzi huo, fundi
mshauri wa Halmashauri ya wilaya ya Tunduru, Hamisi Mpinda aliwataka mafundi wenzake
wanaoendelea na kazi hiyo kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na wataalamu pamoja
na kufuata vipimo husika.
Kadhalika naye mshauri na mfuatiliaji wa miradi ya TASAF wilayani
humo, Christian Amani alisema mradi huo hadi kukamilika ujenzi wake, utagharimu
kiasi cha shilingi milioni 75.
Hata hivyo alieleza kuwa katika kuhakikisha unajengwa na
kukamilika kwa wakati, tayari mfuko huo wa maendeleo ya jamii umekwisha toa
fedha zote na kilicho bakia ni utekelezaji na ukamilishaji wa kazi ya ujenzi
huo.
No comments:
Post a Comment