NAIBU Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto, Dokta Hamis Kingwangalla leo amefanya ukaguzi wa kushitukiza katika Ofisi
za wizara hiyo kwa kusimama getini kuzuia wafanya kazi wote wa wizara, ambao
walikuwa wamefika ofisini baada ya saa 1:30 asubuhi muda ambao ndiyo
mwisho wa wafanyakazi kuingia ofisini.
Awali Dokta Kingwangalla, alifika ofisini hapo saa 1:05
asubuhi huku akiingia ofisini kwa kutembea mwenyewe bila kutumia usafiri wa
gari na kwenda moja kwa moja ofisini kwake, ambapo alitoka ilipofika saa 1:32
na kwenda kusimama getini na kisha kuwaamrisha askari wa geti la kuingia katika
wizara hiyo, kulifunga geti na wasiruhusu mtu yeyote kuingia ndani.
“Fungeni geti na kila atakayefika msimruhusu kuingia ndani,
ninataka kuona wote ambao wanakuja wamechelewa,” alisikika Dokta Kingwangalla
akiwambia askari wa getini.
Baada ya kutoa amri hiyo alimtaka Mkurugenzi wa Utawala na
Rasilimali Watu wa wizara hiyo, Michael John kumpa vitabu vya kusaini kwa
vitengo vyote ili aweke mstari wa kuonyesha kuwa muda wa kuingia ofisini
umekwisha na akafanya hivyo kwa kuweka mstari kwenye vitabu hivyo vya
mahudhurio kuwa muda wa kusaini kuingia umeisha.
Baada ya kukamilisha zoezi hilo, Naibu Waziri alizungumza na
wanahabari kuwa ameamua kufanya zoezi hilo katika ofisi za wizara kwa kutaka
kuona ni jinsi gani watumishi wa ofisi hiyo wamekuwa na mwitikio wa kufanya
kazi kwa kasi anayoitaka Rais, Dokta John Magufuli.
Alisema watumishi hao wameajiriwa na serikali ili kufanya
kazi, lakini wamekuwa wakichelewa kuingia ofisini na yeye kama Naibu Waziri ana
wajibu wa kuwasimamia watumishi hao, ili wafanye kazi ambayo serikali
imewaagiza kufanya.
“Nina wiki moja tangu nimeingia hapa ofisini kuna mambo
ambayo nimeyaona hayapo vizuri na sasa naanza na hili ili tujue kuwa ni akina
nani huwa wanachelewa na zoezi hili litakuwa ni endelevu, kama mimi sitasimamia
watumishi wa serikali basi sitakuwa na kazi wizarani tunataka watumishi ambao
wanakuwa wanafanya kazi kwa kujitoa kwa ajili ya maslahi ya taifa,” alisema Dokta
Kigwangalla.
Aidha Naibu Waziri huyo, alimtaka Mkurugenzi wa Utawala na
Rasilimali Watu kuhakikisha watumishi wote waliochelewa kufika ofisini
wanaandika barua ya kutoa maelezo kwanini wanachelewa kufika ofisini na baada
ya hapo, Mkurugenzi na yeye atoe maelezo kwanini muda wa kutoka watumishi
wanakuwa hawasaini kuwa wametoka.
Pia alishauri uongozi wa Wizara, ufanye mabadiliko ya mfumo
wa watumishi kuingia ofisini kwa kutumia mifumo ya kisasa ya kadi au kidole
“Biometric” ili kuwa na taarifa katika mifumo ya mawasiliano kujua wanaochelewa
ofisini na wanaowahi kutoka na baada ya hapo, uongozi utajadili adhabu za
kuwapa watumishi wote ambao wamekuwa wakichelewa kufika na kuwahi kutoka
ofisini.
No comments:
Post a Comment