Na Bashir Yakub,
MARA kadhaa linapoibuka suala la
kugawana mali pale ndoa inapohesabika
kushindikana masuala kadhaa ya msingi
na yanayohitaji uelewa huwa yanaibuka. Moja
ya suala kati ya masuala ambayo
huibuka ni hili la kutenganisha na kufafanua
hadhi ya mali za wanandoa ili mgawanyo
uweze kufanyika kwa haki.
Yawezekana mwanandoa akadhani ana
haki katika mali fulani lakini kumbe
kisheria hana haki hiyo ni mtazamo wake
ndio unamsukuma kuamini hivyo.
Halikadhalika
yawezekana mwanandoa hudhani hana haki
katika mali fulani kumbe anayo haki. Ili
kujua una haki ipi katika mali
ipi na huna haki katika mali ipi
yahitajika kujua misingi ya kisheria inayotumika
kugawanya mali za wanandoa.
1. KUGAWANA MALI ZA WANANDOA
Ieleweke kuwa tunapoongelea wanandoa
kugawana mali tunaongelea talaka. Hakuna kugawana
mali bila talaka. Na kisheria talaka
inapotoka tu swali linalofuata ni habari ya mali
na watoto kama wapo. Mali si lazima
magari na manyumba lakini pia hata vyombo
vya ndani vikiwemo vitanda, makabati, sahani n.k
nazo ni mali kwa mujibu wa sheria.
Navyo huhitaji mgao.
2. JE KUGAWANA MALI NI
NUSU KWA NUSU ?
Linapokuja suala la kugawana
mali wengi hudhani mtindo unaotumika kugawa ni
ule wa nusu kwa nusu. Jambo
hili si kweli kwakuwa sheria ya ndoa 1971
iliyofanyiwa marekebisho 2002 haisemi kuwa
utaratibu wa kugawana mali ni nusu kwa
nusu.
Sheria hii imeweka msingi mkuu wa
kugawana mali ambao ndio hutumika katika Mahakama
zetu katika kutoa maagizo ya kugawana
mali za wanandoa.
Msingi uliowekwa na sheria ni
msingi wa kiwango cha mchango wa
mwanandoa katika kupatikana kwa mali husika.
Kiwango alichochangia mwanandoa katika kupatikana
kwa mali hiyo ndicho kitakachokadiriwa na
kiwango hicho ndicho atakachopewa. Kwa hiyo kama ni
nyumba ya vyumba sita mmoja anaweza kupata
chumba kimoja na mwingine akapata vitano
kutegemea na mchango wake.
Na mchango hapa
sio leta ni lete. Mchango sio hela tu
hata kazi za nyumbani anazofanya mama
wa nyumbani ambaye haleti hela nazo
huitwa mchango ambapo hukadiriwa na kupata
kile anachostahili.
3. MALI KABLA YA NDOA NA
BAADA YA NDOA
Katika kutenganisha mali za
wanandoa huwa zinatenganishwa katika
makundi makuu matatu. Kwanza
kuna mali ambazo mtu alikuwa nazo kabla ya
ndoa na wakati anaingia katika ndoa
ameingia nazo. Kwa mfano mwanamke ameolewa
akamkuta mwanaume tayari ana nyumba yake.
Pili kuna mali ambazo zimepatikama wakati
wawili wakiwa katika ndoa.
Kwa mfano ndoa imefungwa wawili
wakaanza kuishi pamoja na taratibu wakaanza kujenga
na kukamilisha. Na tatu ni mali ambazo
zimepatikana katika ndoa lakini zikiwa hazina
uhusiano wowote wa kindoa kwa mfano kurithi
au kuzawadiwa mali. Tutaona hapa chini mazingatio
ya sheria ya kila moja katika haya.
4. JE MALI
ILIYOPATIKANA KABLA YA NDOA INAHESABIKA NI
YA FAMILIA
Mali iliyopatikana kabla ya ndoa
na ikaendelea kuwepo kipindi cha ndoa
inaendelea kuwa ya huyo mwenye nayo bila
ushirika wa mwenza wake. Kama ni nyumba
mwanamke alikuwa nayo kabla ya kuolewa
au ni mwanaume alikuwa nayo kabla ya
kuoa basi inaendelea kuwa ya kwake peke
yake na haihusiki katika mgao suala
la mgao linapojitokeza.
Hata hivyo inaweza kuingizwa
katika mgao ikiwa kuna mchango wowote wa
kuiendeleza ulitolewa na mwenza. Kwa mfano kabla
ya ndoa ilikuwa na vyumba viwili lakini
katika kipindi cha ndoa imepanuliwa na
kufikia vyumba vitano, au ilikuwa haina
uzio, au haina madirisha kabla ya ndoa
lakini baadae vitu hivyo vikawepo. Katika
hali kama hiyo itatakiwa iingizwe katika
mgao na kutazama kiwango cha mchango wa kila
mmoja katika uendelezaji huo. Ni hapo
ambapo mchanganuo utafanyika ili kila mmoja
apate haki kutokana na kiwango cha
mchango wake.
Ikiwa hakuna uendelezaji wowote
uliofanyika katika mali yaani labda nyumba
ilivyokuwa kabla ya ndoa ndivyo hivyo hivyo
ilivyoendelea kubaki hata baada ya ndoa
basi mali hiyo haitatakiwa kuingizwa katika
mali za mgao bali itabaki mali ya
mwanandoa mmoja pekee ambaye ndiye mmiliki
wa tangu awali.
Hali ni hiyo hiyo hata kwa
mali ambayo imepatikana katika ndoa lakini
ikiwa haina uhusiano na kipato cha
wanandoa, kwa mfano mali ya urithi au zawadi.
Hii ina maana ikiwa mali hii itaendelezwa
basi mchango wa uendelezaji utatathiminiwa na
ikiwa haitaendelezwa basi itabaki mali ya
mrithi au mpewa zawadi pekee na
haitahusu mgao.
MWANDISHI WA MAKALA HAYA
NI MWANASHERIA NA MSHAURI WA
SHERIA KUPITIA GAZETI LA SERIKALI LA
HABARI LEO KILA JUMANNE, GAZETI
JAMHURI KILA JUMANNE NA GAZETI
NIPASHE KILA JUMATANO.
0784482959,
0714047241 bashiryakub@ymail.com
No comments:
Post a Comment