Na Bashir Yakub,
KAWAIDA wanandoa wengi wanapoingia
katika migogoro moja ya jambo
wanalokimbilia kama jawabu la mgogoro ni talaka.
Kwa misingi ya ndoa za kiislamu
talaka huruhusiwa tofauti na misingi ya
ndoa za kikiristo ambazo talaka huwa
haziruhusiwi. Hata kama ndoa ni ya
kikristo ambayo hairuhusu talaka linapokuja suala
la Mahakama basi hata ndoa hizo nazo
hutolewa talaka. Ieleweke
kuwa kwa mujibu wa sheria ya ndoa ya mwaka 1971
suluhu ya kumaliza utata katika ndoa
si talaka tu.
Na hii ni kutokana na umuhimu wa
ndoa. Katika hili sheria ya ndoa imetoa chaguo
jingine ambalo mtu anaweza kulitumia kama
mbadala wa talaka. Hili linahusu kutengana
kama tutakavyoona.
1.KUTENGANA KISHERIA.
Kutengana kwa mujibu wa
sheria ni hatua ambayo watu wawili mwanamke
na mwanaume walio katika ndoa halali huamua
kutoshirikiana katika mambo kadhaa ya kindoa huku
ndoa ikihesabika kuwa haijavunjika. Katika hili
kinachositishwa ni baadhi ya haki na wajibu wa
kindoa. Lakini kusitishwa kwa wajibu na haki
hizo hakuhesabiki kuwa kumevunja ndoa.
2. AINA ZA KUTENGANA KISHERIA.
Kisheria zipo njia mbili ambazo
wanandoa wanaweza kutumia ili kutengana.
Kwanza ni kuwa wanandoa wanaweza kutengana
wenyewe kwa hiari yao. Kutengana kwa
hiari ni kuwa wanakubaliana kutengana kwa
muda fulani kutokana na kutoelewana kwasababu
mbalimbali za kifamilia.
Pili wanaweza kutengana kwa
kutenganishwa na Mahakama kwa mujibu wa
kifungu cha 99 cha sheria ya ndoa mwaka 1971.
Hii ni baada ya mmoja
wa wanandoa kuiomba Mahakama iwatenganishe
kwa kipindi fulani na Mahakama kuridhika
kuwa ipo haja hiyo.
Mara nyingi kutengana kwa njia ya Mahakama
hutokea baada ya hatua za kutengana
kwa hiari kushindikana. Mara kadhaa
hutokea ambapo mmoja wa ndoa huwa amekerwa
na baadhi ya tabia na hivyo kumuomba
mwenzake watengane ambapo mwenzake hukataa.
Inapotokea hivyo ndipo mwanandoa anapolazimika
kukimbilia Mahakamani kuomba kutengana.
3. TOFAUTI YA KUTENGANA NA TALAKA.
Talaka ni hatua ambapo
ndoa hutangazwa kuwa imevunjika kabisa na
kila mmoja hutakiwa kuendelea na maisha yake. Talaka huambatana
na haki ikiwemo ile ya mgawanyo wa
mali. Wakati kutengana ni hatua ya
kuchana kwa muda na kurudiana baadae.
Kutengana hakuambatani na haki ya kugawana mali
za machumo ya wanandoa.
4. UMUHIMU WA KUTENGANA BILA TALAKA.
Sheria imeelekeza tendo hili la
kutengana kwa kuzingatia maslahi mapana ya
wanandoa, familia na jamii kwa ujumla.
Lengo kuu la hatua ya kutengana ni
kutoa nafasi kwa walengwa wanandoa kujirekebisha.
Inaaminika kuwa katika
kipindi ambacho wanandoa hutengana huwa
kuna mwanya mkubwa ambao hupelekea
kurekebisha baadhi ya tabia ambazo zilikuwa
kikwazo. Kutengana ni nafasi ya mtu kujirudi.
5. MATUNZO YA MWANAMKE NA
WATOTO KIPINDI CHA KUTENGANA.
Kwa upande wa mwanaume ni
lazima kwake kuendelea kutoa matunzo ya
mwanamke pamoja na ya watoto kama wapo. Kisheria
mwanaume ndiye huwajibika kutoa matumizi ya
watoto pamoja na kumtunza mke wake.
Katika kipindi cha kutengana haki
na wajibu huu huendelea mpaka kipindi cha
kutengana kitakapoisha. Hata hivyo yapo mazingira
ambapo mwanamke anaweza kutakiwa kutoa
matunzo kwa mwanaume kama itakavyokubaliwa katika
masharti ya kutengana.
6. MUDA WA KUTENGANA.
Kawaida (practice) muda wa kutengana
unaotakiwa inabidi iwe miaka miwili
na ikizidi isizidi mitatu. Ikiwa muda huo
utapita bila muafaka kwa wahusika basi
hatua za talaka zinaweza kufuata.
7. KUAMUA KUSITISHA MUDA WA KUTENGANA.
Kifungu cha 113 ( 1 ) kinatoa uhuru
kwa wanandoa kutuma maombi ya pamoja Mahakamani
kuomba kusitishwa kwa amri ya kutengana.
Hii ni ikiwa kutengana kulitokana na amri
ya Mahakama. Ikiwa kutengana hakukutokana na Mahakama
ila ilikuwa kwa ridhaa ya wanandoa basi
wahusika kwa hiari yao wanaweza kuamua
kusitisha bila amri ya Mahakama.
MWANDISHI WA MAKALA
HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI
WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA SERIKALI
LA HABARI LEO KILA JUMANNE, GAZETI
JAMHURI KILA JUMANNE NA GAZETI
NIPASHE KILA JUMATANO.
0784482959,
0714047241
bashiryakub@ymail.com
No comments:
Post a Comment