Tuesday, November 17, 2015

KATIBU WA SIASA NA UENEZI MKOA WA RUVUMA ALALAMIKIWA NA WAGOMBEA


Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

MPASUKO mkubwa huenda ukajitokeza na kukikumba Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, kufuatia Katibu wa siasa na uenezi wa mkoa huo, Benedict Ngwenya kuonekana wazi akiweka mikakati ya kupanga safu za wagombea wa nafasi ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Mbinga wilayani humo.

Kigogo huyo wa CCM ambaye pia naye ameomba kugombea nafasi hiyo, anadaiwa kupita katika maeneo mbalimbali mjini hapa na kuwatisha baadhi ya wagombea wenzake kwamba, yeye ndiye mwenye uwezo wa kuongoza nafasi hiyo na sio mwingine.

Kufuatia kuwepo kwa malalamiko hayo, imeelezwa kuwa kitendo hicho kinachofanywa na Ngwenya, ni utovu wa nidhamu ndani ya chama ambapo viongozi wenye mamlaka ya uteuzi majina ya wagombea wa nafasi hiyo ngazi ya mkoa, endapo hawatazingatia taratibu husika huenda kukatokea mpasuko mkubwa kwa madiwani wanaotarajia kuunda Halmashauri hiyo mpya, ya mji wa Mbinga.


“Huyu mgombea mwenzetu tunamshangaa sana, kwa muda mrefu amekuwa akipita kutamba mitaani yeye ni mjumbe wa kamati ya siasa ya mkoa wa Ruvuma, atahakikisha jina lake katika uteuzi linarudi pamoja na majina mengine anayoyataka yeye ili aweze kujipatia chapuo la ushindi katika nafasi hii ya uenyekiti”, alisema mmoja kati ya wagombea ambaye aliomba jina lake lisitajwe.

Walisema mpaka sasa bado wanaimani na vikao vya uteuzi ngazi ya mkoa, ambavyo vinatakiwa kutenda haki na sio kumsikiliza mtu mmoja ambaye kimsingi anaonesha wazi, kutaka kuvuruga uchaguzi huo.

Ngwenya wamemnyoshea kidole pia amekuwa ni mtu mwenye dharau, na kwamba hata anapopewa ushauri ambao mbele yake una maslahi makubwa katika chama amekuwa akipuuza, hivyo wakati umefika kwa Chama Cha Mapinduzi kuweka kando viongozi wa aina hiyo ambao wanaweza kulipeleka Taifa mahali pabaya.

Kadhalika walifafanua kuwa Halmashauri ya mji wa Mbinga ni changa imeanzishwa mwaka huu, hivyo ni vyema wakachaguliwa viongozi ambao watakuwa na upeo mkubwa wa kuongoza na kubuni vyanzo vya kuiingizia mapato ili kuweza kusukuma gurudumu la maendeleo ya wananchi.

Vilevile kwa upande wao baadhi ya wananchi kwa nyakati tofauti mjini hapa, wametoa maoni yao wakisema madiwani wanaounda Halmashauri hiyo wanapaswa kuwa makini kwa kumchagua Mwenyekiti na makamu wake, ambao watakuwa na uwezo wa kuongoza na sio ambao watakuwa na uroho wa madaraka wakipenda kujilimbikizia mali wao wenyewe.

Pamoja na mambo mengine, nao wadau mbalimbali wa vyama vya siasa walisema uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25 mwaka huu umepita, na kwamba kinachotakiwa sasa kwa madiwani katika kata husika kuhakikisha wanatekeleza kwa vitendo majukumu ya wananchi na sio vinginevyo.

Mwandishi wa habari hizi, alipozungumza na Ngwenya juu ya malalamiko hayo ambayo ananyoshewa kidole na madiwani wenzake wa Halmashauri ya mji wa Mbinga,  alikataa kuzungumzia lolote huku akiongeza kuwa hana nafasi amebanwa na mambo mengi ambayo anapaswa kuyatekeleza.

Wagombea wanaowania kwa nafasi ya Mwenyekiti katika Halmashauri ya mji huo, kwenye mabano na kata walizotoka kuwa ni Christantus Mbunda (Kagugu), Ndunguru Kipwele (Myangayanga), Raphael Kambanga (Masumuni), Lenard Robert (Matarawe), Aureus Ndunguru (Luwaita), David Mapunda (Ruhuwiko) na Benedict Ngwenya kutoka kata ya Mpepai.

Hata hivyo kwa nafasi ya makamu Mwenyekiti mgombea ni, Aurelia Ntani (Mbinga mjini), Imelda Mapunda diwani viti maalumu (Mbinga mjini), Costansia Mawondo diwani viti maalumu (Mbinga mjini), Grace Madeleke diwani viti maalumu (Mbinga mjini) na Tasilo Ndunguru kutoka kata ya Kikolo.

No comments: