Mkuu wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Senyi Ngaga. |
Na Muhidin Amri,
Mbinga.
SERIKALI wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, imewaagiza watendaji
wake wa Halmashauri ya wilaya hiyo kuandaa mkakati madhubuti wa kuongeza vyanzo
vya mapato, vitakavyowezesha halmashauri hiyo kupata fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji
wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Rai hiyo ilitolewa juzi na Mkuu wa wilaya hiyo, Senyi Ngaga
alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu ofisini kwake mjini hapa.
Ngaga alisema, Halmashauri ya Mbinga kwa kiasi kikubwa bado
inaendelea kutegemea ruzuku kutoka serikali kuu kutokana na kukosa vyanzo
vikubwa vya mapato na hata vilivyokuwepo, kumekuwa na udhaifu mkubwa wa
usimamizi jambo ambalo linalotoa nafasi kwa wajanja wachache kutumia nafasi
hiyo kujinufaisha.
Alisema kuwa kutokana na udhaifu huo, halmashauri
haiwezi kujiendesha katika mambo yake yenyewe na hivyo itaendelea kutegemea
serikali au wafadhili, jambo ambalo ni hatari kwa sababu pindi
serikali itakapowataka kujitegemea kwa kila jambo, itakuwa vigumu kulipa hata
mishahara ya watumishi wake.
Kwa mujibu wa Ngaga, alifafanua kuwa hali hiyo inatokana
na uwezo mdogo wa watendaji pamoja na madiwani kuwa na uwezo mdogo wa kubuni na
kutafuta vyanzo vipya vya mapato, ambapo matokeo yake huendelea kutegemea vya
zamani ambavyo wanashindwa kuvisimamia vizuri ili waweze kupata mapato makubwa
yatakayosaidia kuendesha shughuli zao za kila siku.
“Baadhi ya watendaji tulionao hawapo makini katika kutekeleza
majukumu yao, licha ya wilaya kubarikiwa katika uzalishaji wa mazao ya kila
aina, lakini bado tupo nyuma ukizingatia kwamba uzalishaji wa mazao ni mkubwa”,
alisema Ngaga.
Aliongeza kuwa, kupitia malengo waliyonayo amewataka kuwa
makini hasa katika eneo la kuongeza mapato kupitia vyanzo vilivyopo
ambapo kama vitasimamiwa vizuri vitaleta manufaa kwa halmashuri na
kupiga hatua ya kimaendeleo kama ilivyokuwa kwa halmashauri nyingine hapa
nchini.
Kadhalika alibainisha kwamba ni ukweli usio na mashaka kuwa
Mbinga, ni kati ya wilaya zilizobahatika kuwa na raslimali nyingi ambazo kama
watendaji wake na wananchi kwa ujumla, watazifanyia kazi ipasavyo halmashauri
itaweza kupiga hatua mbele zaidi.
No comments:
Post a Comment