Tuesday, February 18, 2014

HALMASHAURI YA MBINGA YAINGIA MKATABA WA MAFUNZO YA KUTENGENEZA VITO VYA THAMANI, WAKOREA KUJENGA KIWANDA

Mbunge wa jimbo la Mbinga Gaudence Kayombo(aliyesimama) akisisitiza jambo wakati wa kumkaribisha mtaalamu wa madini kutoka Korea, Dokta Kim (katikati) ambaye ana lengo la kupanua soko la madini kwa wachimbaji wadogo wadogo wa madini na kutangaza fursa za kimaendeleo kwa mataifa mengine wilayani Mbinga. Kushoto ni mtaalamu mwenzake aitwaye Changlee.



Mtaalamu wa madini ambaye ni wa kwanza kutengeneza vito vya thamani Korea kusini Dokta Kim, (kushoto) akiweka sahihi katika mkataba aliotiliana nao na Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma katika hafla fupi iliyofanyika ukumbi wa chuo cha maendeleo uliopo mjini hapa, Upande wa kushoto kwa Dokta Kim ni mkuu wa chuo cha maendeleo ya jamii (FDC) wilayani Mbinga Aidan Mchawa naye akiweka sahihi katika mkataba huo wa kutoa mafunzo ya kutengeneza vito hivyo na kujenga kiwanda cha kutengeneza vito vya thamani wilayani humo, kiwanda hicho kinatarajiwa kujengwa na wakorea hao miaka mitano ijayo. Wanaoshuhudia kutoka kushoto ni Askofu wa jimbo la Mbinga John Ndimbo na anayefuatia ni Mbunge wa jimbo la Mbinga Gaudence kayombo. (Picha na Kassian Nyandindi)

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
 
HALMASHAURI ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma kupitia chuo chake cha maendeleo ya jamii (FDC) kilichopo mjini hapa, kimeingia mkataba na mtaalamu wa madini ambaye anafahamika kwa jina la Dokta Kim kutoka nchi ya Korea kusini, kwa ajili ya kutoa mafunzo ya wiki mbili ya utengenezaji wa vito vya thamani.
 
Pia mkataba huo unalenga miaka mitano ijayo mtaalamu huyo ataweza kujenga kiwanda cha kutengeneza vito vya thamani wilayani humo, jambo ambalo litaweza kupanua soko la ajira kwa wananchi wa wilaya hiyo.
 
Akizungumza katika hafla fupi ya kutiliana sahihi katika ukumbi wa chuo cha maendeleo uliopo Mbinga mjini, Dokta Kim alisema yeye ni mtu wa kwanza katika nchi hiyo ya Korea kusini ambaye anaongoza kwa utengenezaji wa vito vya thamani, hivyo anawaomba washiriki walioteuliwa kujiunga na mafunzo hayo kuwa makini wakati watakapo kuwa darasani.
 
Dokta Kim alisema kuwa wazo hili la kuja Mbinga na kutaka kufanya hayo ni jitihada zilizofanywa na Mbunge wa jimbo la Mbinga Gaudence Kayombo, ambapo mafunzo hayo yataweza kuwafungua vijana wa wilaya hiyo waweze kufanya shughuli za utengenezaji wa vito hivyo na kuweza kuondokana na umasikini.
 
Washiriki wa mafunzo hayo wapo 20 kutoka katika maeneo mbalimbali wilayani humo ambako madini yanachimbwa, wametakiwa mara baada ya kumaliza kupata ujuzi wa kutengeneza vito vya thamani kama vile pete, bangili, heleni na hata mikufu ya kuvaa shingoni waache ubinafsi badala yake elimu hiyo waieneze kwa wengine.
 
“Naomba muwe na moyo wa kupokea mafunzo haya kwa faida ya jamii ya wanambinga, soko la vito vya thamani lipo jambo la msingi ni kutengeneza vito vyenye ubora wa hali ya juu”, alisisitiza Dokta Kim.
 
Vilevile kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Mbinga Gaudence Kayombo alisema lengo la kumleta mtaalamu huyo wa madini, ni kutaka pia kupanua soko la madini kwa wachimbaji wadogo wadogo wa madini na kutangaza fursa za kimaendeleo kwa mataifa mengine wilayani humo.
 

No comments: