Tuesday, February 11, 2014

MBINGA NAKO KWA CHAFUKA WAFANYABIASHARA WAGOMA

Jakaya Kikwete, Rais wa Tanzania.

 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
 
HALI  si shwari  katika  mji  wa Mbinga mkoani Ruvuma, kufuatia  kuanza kwa mgomo  usio na kikomo wa wafanyabiashara kama njia ya  kufikisha ujumbe  kwa Waziri wa viwanda na biashara   na  serikali ya  Rais Jakaya  Kikwete,  juu ya gharama za mashine za kutolea risiti (EFD) wakidai kwamba gharama hizo ni kubwa na ni sawa na kumtishwa mzigo mfanyabiashara ambao hauna tija kwake.  


Mgomo huo umeanza leo  asubuhi  hii  huku  makundi ya wafanyabiashara wakiwa wamekusanyika katika maeneo mbalimbali ya mji huo, huku wakipanga kufanya maandamano  kuwaadhibu wenzao wanaokiuka mgomo huo ambao wataonekana wamefungua maduka.


Hali kwa upande wa wakazi wa Mbinga mjini  na wale wa maeneo ya vijijini ambao  wanakuja kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali imewafanya wawe katika wakati mgumu kutokana na mgomo huo, hivyo kujikuta wakiambulia makufuri katika maduka hayo.


Wafanyabiashara  hao  wametoa onyo kwa  wenzao iwapo  watafungua  maduka yao  watakiona cha moto  na  kuanzia  wakati  wowote sasa,  wataanza msako wa duka moja hadi jingine kwani wamesema mgomo  huo ni wa nchi nzima na wao  wametii uamuzi wa  wafanyabiashara wenzao katika mikoa yote iliyopo hapa nchini.
 

Mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga alipotafutwa na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu, ili aweze kuzungumzia suala hilo alisema wapo kwenye kikao wanajadili tatizo hilo hivyo atalitolea taarifa baadae.
 

“Hivi sasa nipo kwenye kikao tunajadili suala hili naomba nitafute baadae kidogo tutaweza kuzungumza”, alisema.
 

Hata hivyo hadi habari hizi zinaingia mitamboni bado hali ilikuwa tete ambapo makundi ya wafanyabiashara wa aina mbalimbali katika mji wa Mbinga, yalikuwa bado yakiendelea kuonesha msimamo kwamba hawataweza kufungua maduka yao wakidai kwamba wanapinga gharama kubwa za mashine hizo za kutolea risiti huku wakiongeza kuwa ni vyema serikali, ikasikiliza kilio chao na kukifanyia kazi kwa kupunguza gharama hiyo.

No comments: