Friday, February 21, 2014

POLISI WAFANIKIWA KUKAMATA JAMBAZI LILILOKUWA LIKITESA WANANCHI WA MBINGA KWA MUDA MREFU

Jambazi linalodaiwa kuwa sugu Roster Ndunguru (katikati) akiwa chini ya ulinzi wa polisi katika hospitali ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, ambako amelazwa baada ya kuambulia kipigo kutoka kwa Polisi wakati akijaribu kutoroka.

Jambazi linalodaiwa kuwa sugu Roster Ndunguru (27) mkazi wa kijiji cha Mbangamao akiwa amefungwa pingu katika hospitali ya wilaya ya Mbinga ambako amelazwa baada ya kuambulia kipigo kikali kutoka kwa Polisi wakati akijaribu kutoroka mikononi mwao. (Picha zote na Kassian Nyandindi)



Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

JESHI la Polisi wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, limefanikikwa kumkamata Roster Ndunguru mkazi wa kijiji cha Mbangamao wilayani humo ambaye anadaiwa kuwa ni jambazi sugu na amekuwa akifanya matukio mengi ya kiuhalifu ikiwemo kuwajeruhi watu na kunyang’anya mali zao.

Aidha Jambazi hilo lilikuwa likitafutwa kwa muda mrefu baada ya kumjeruhi Mratibu elimu kata ya Mbangamao, Florence Kowelo kwa kumjeruhi sehemu mbalimbali za mwili wake na kumpiga na kitu kizito kichwani.

Tukio hilo imeelezwa kuwa lilitokea majira ya usiku wakati Mratibu huyo akiwa nyumbani kwake amelala na familia yake, ambapo baada ya kupiga kelele majirani walijitokeza na jambazi hilo lilitokomea kusikojulikana.

Kwa mujibu wa chanzo cha uhakika kutoka Jeshi la Polisi wilayani Mbinga ambacho hakikutaka jina lake litajwe katika mtandao huu, kilisema kuwa Roster amekuwa na matukio mengi ya kiujambazi ambayo amekuwa akiyafanya katika maeneo mbalimbali wilayani humo.


Alisema amekuwa akitembea nyakati za usiku na silaha kama vile panga, nondo ambavyo amekuwa akivitumia kujeruhi watu kisha kupora mali zao.

Pamoja na mambo mengine alifafanua kuwa mafanikio ya kuweza kumkamata yalitokana na jeshi hilo kupata taarifa kutoka kwa raia wema kwamba jambazi hilo, lilikuwa likiranda randa katika kijiji cha Mbangamao wilayani humo ndipo polisi walikwenda huko majira ya usiku wa Februari 20 na kuweza kufanikiwa kumkamata.

Hata hivyo kaimu Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma, Revocatus Malimi alipotafutwa ili aweze kuzungumzia juu ya tukio hilo hakuweza kupatikana na kwamba Jambazi hilo limelazwa katika hospitali ya wilaya hiyo, akiugulia majeraha baada ya kuambulia kipigo wakati akijaribu kutoroka mikononi mwa Polisi.


No comments: