Monday, February 24, 2014

MAFUNZO YA UTENGENEZAJI VITO VYA THAMANI MBINGA YAKAMILIKA, WASHIRIKI WAIOMBA SERIKALI KUUNGA MKONO

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
 
WASHIRIKI wa mafunzo ya kutengeneza vito vya thamani wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wameiomba serikali wilayani humo kuendelea kuunga mkono mafunzo waliyoyapata ili yaweze kuleta faida kwa kizazi cha sasa na kijacho.
 
Kauli hiyo ilitolewa kupitia risala yao iliyosomwa na mmoja kati ya washiriki hao, Editha Komba mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa wilaya hiyo Senyi Ngaga wakati wa kufunga mafunzo hayo ya wiki mbili yaliyofanyika katika chuo cha maendeleo ya wananchi (FDC) kilichopo mjini hapa.
 
Aidha katika risala hiyo washiriki hao walisema wameweza kujifunza kutengeneza ukataji wa vipande vya aluminiamu na shaba, kutengeneza mapambo mbalimbali kama vile heleni, cheni na bangili.
 
Walieleza kuwa wameweza kujifunza kutumia vitu vya asili kama vile mbegu za maembe, kahawa, maboga na manyoya ya kuku kutengeneza mapambo ya asili.
 
Komba aliongeza kuwa wakati wanajifunza waliweza kupata changamoto mbalimbali ikiwemo uchache wa vifaa vya kufundishia hivyo walimuomba mkufunzi wa mafunzo hayo Profesa Kim, kutoka nchi ya Korea kusini kuhakikisha kwamba wakati ujao mafunzo hayo yatakapotolewa tena wilayani Mbinga kuwepo na vifaa vya kutosheleza mahitaji halisi.
 
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya hiyo Ngaga, aliwataka washiriki wa mafunzo hayo huko waendako wakayaendeleze kwa wengine ili jamii kwa ujumla iweze kunufaika nayo.
 
Hata hivyo alieleza kuwa serikali itaendelea kuunga mkono jitihada zinazofanywa na taasisi mbalimbali ikiwemo vyuo vya ufundi nchini ambavyo hutoa mafunzo yanayolenga wahitimu kujiajiri wao wenyewe na hivyo kusaidia jamii kuondokana na ukosefu wa ajira.
 

No comments: