Ofisi za makao makuu ya Kampuni ya Tutunze Kahawa Limited (TKL) zilizopo Mbinga mjini. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WADAU wa maendeleo wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma
wameipongeza Kampuni ya Tutunze Kahawa Limited (TKL) iliyopo wilayani hapa, kwa
jitihada zake za kuunga mkono na kuchangia shughuli mbalimbali za maendeleo ya
wananchi wilayani humo.
Pongezi hizo zilitolewa juzi mjini hapa, wakati kampuni hiyo
ilipokuwa ikikabidhi madawati 20 yenye thamani ya shilingi milioni 1.9 kwa
uongozi wa halmashauri ya wilaya hiyo kwa ajili ya kukalia wanafunzi shuleni.
Walisema kuwa juhudi hizo zinazofanywa na TKL kuna kila
sababu kwa makampuni mengine yaliyopo wilayani Mbinga, kuiga mfano huo katika
kuchangia michango ya maendeleo ili wilaya hiyo iweze kusonga mbele na kukua
kiuchumi.
Aidha naye Meneja masoko wa kampuni hiyo, Thomas Ngapomba kwa
upande wake alisema kuwa katika juhudi za kuunga mkono kampeni iliyoanzishwa na
Rais Dkt. John Magufuli ya kuondoa tatizo la madawati kwa shule za msingi na
sekondari hapa nchini, Tutunze Kahawa Limited nayo iliona kuna umuhimu wa kuchukua
jukumu la kuchangia madawati hayo kwa wilaya ya Nyasa na Mbinga.
Ngapomba alifafanua kuwa lengo la kufanya hivyo ni
kuhakikisha kwamba wanafunzi wanakuwa na mazingira mazuri ya kusomea, pale
wanapokuwa darasani ili waweze kuandika mwandiko mzuri.