Na Kassian Nyandindi,
Songea.
AGIZO limetolewa kwa Watendaji wote wa Halmashauri za wilaya
ya Songea mkoani Ruvuma, kuhakikisha kwamba wanawapiga faini wananchi ambao wataonekana
kutotii amri ya kufanya usafi kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi ili iweze kuwa
fundisho kwa wengine na kuleta mabadiliko chanya, kwa jamii kujenga tabia ya
kufanya usafi katika maeneo yao.
Mkuu wa wilaya ya Songea, Palolet Mgema alitoa agizo hilo
juzi wakati alipokuwa akizungumza na wakazi wa mtaa wa Miembeni kata ya Bombambili
mjini hapa, ambako shughuli za usafi wa mazingira kiwilaya zilikuwa zikifanyika
na kuongozwa naye.
Kwa ujumla wilaya hiyo inaundwa na halmashauri tatu ambazo ni
Manispaa ya Songea, halmashauri ya wilaya ya Songea na ile ya Madaba.
Mgema alisema kuwa watu wote ambao hawataki kufanya usafi wa
mazingira kuanzia sasa watozwe faini ya shilingi 50,000 na kwamba anataka
ripoti ya watu hao pale wanapotozwa ifikishwe ofisini kwake haraka, ili aweze
kutambua ni nani wenye tabia ya kugoma kufanya usafi ili waweze kuchukuliwa
hatua zaidi.