Wednesday, November 13, 2013

UHARIBIFU WA MAZINGIRA NA UCHOMAJI MOTO MISITU WATISHIA KUTOWEKA KWA VYANZO VYA MAJI RUVUMA

Mazingira yanavyoharibiwa kama hivi, ni hatari kwa maisha ya binadamu na viumbe hai. 

Na Kassian Nyandindi,
Songea.

WANANCHI waishio mkoani Ruvuma, wameshauriwa kuwa na tabia ya kutunza mazingira pamoja na vyanzo vya maji na kuvifanya kuwa endelevu, kwa  faida ya vizazi vijavyo na hata kwa matumizi yao wenyewe ili waweze kuwa na maisha endelevu.

Hivi sasa kumekuwa na kasi kubwa ya uharibifu wa vyanzo hivyo kunakosababishwa na shughuli za kibinadamu kama vile kilimo na ufugaji hali ambayo inatishia kutoweka kwa uoto wa asili.

Wito huo ulitolewa na mshindi wa tuzo ya mazingira ambaye pia ni mwanaharakati  wa msuala ya mazingira na uhifadhi wa vyanzo vya maji mkoani Ruvuma, Menas Andoya alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Songea, kuhusiana na kasi  kubwa ya uchomaji  moto misitu na uchafuzi wa vyanzo vya maji ambao umeshamiri mkoani humo.

Alisema viongozi kuanzia ngazi ya vitongoji, vijiji   na hata kata wanapaswa kusimamia kikamilifu suala la utunzaji wa mazingira pamoja na vyanzo vya maji kutokana na wao ndiyo wanaoishi na wananchi.


“Kila siku baadhi ya wananchi kazi yao ni kukata miti na kulima katika vyanzo vya maji ambavyo ni tegemeo kubwa kwa maisha ya binadamu na wanyama hai, inatakiwa sasa jamii ibadilike ili tuweze kuondokana na ukame unaoweza kujitokeza hapo baadaye”, alisema Andoya.

Vilevile amesikitishwa na hali ya mazingira ilivyo katika wilaya mbalimbali hapa mkoani Ruvuma, ambapo wananchi wanachoma moto misitu na kukata miti kwa wingi ambayo ni tegemeo kubwa kwa mvua ili iweze kunyesha huku wakishindwa kupanda mingine na kusababisha maeneo mengi kuwa jangwa.

Alifafanua kuwa kutokana na utafiti alioufanya miaka kadhaa iliyopita, amebaini kuwepo kwa  baadhi ya viongozi wa ngazi za chini yaani vijiji na kata kuwa wamekuwa wakishiriki katika uharibifu huo, na kuwahamasisha wananchi kulima kwenye vyanzo vya maji kwa maslahi yao binafsi ya kisiasa na kutaka umaarufu usiokuwa na faida kwa watu wengine.

Andoya alisema,tabia hiyo imechangia sana kuwepo kwa uhaba mkubwa wa maji katika maeneo mbalimbali, na kama  hakutakuwa na hatua madhubuti zitakazochukuliwa katika kudhibiti hilo, hali inaweza kuwa mbaya zaidi.


Pamoja na mambo mengine ameishauri serikali kupitia mamlaka husika za maji  na mazingira mkoani Ruvuma, kuendesha semina za utunzaji wa mazingira na vyanzo vya maji hususani maeneo ya vijijini  ambako ndiko kwenye idadi kubwa ya waharibifu wa vyanzo vya maji na mazingira.

No comments: