Sunday, November 3, 2013

BARAZA LA MADIWANI WILAYANI MBINGA LAMSHUSHIA RUNGU AFISA ELIMU TAALUMA, WAMKATAA WATAKA AREJESHWE KWA KATIBU MKUU WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Shukuru Kawambwa.














Na Kassian Nyandindi,
Ruvuma.


HATIMAYE Baraza la Madiwani katika Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, limefanya maamuzi mazito ya kumkataa Afisa Elimu Taaluma wa wilaya hiyo Rashid Pilly, na kumwagiza Mkurugenzi na Mwenyekiti wake wa halmashauri hiyo kumwondoa haraka afisa huyo na kumrejesha kwa Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya ufundi.


Pilly analalamikiwa kwa muda mrefu kutokana na kile kinachoelezwa kuwa ni kikwazo katika utendaji kazi wa idara hiyo, amekuwa akitumia muda mwingi badala ya kufanya kazi husika, yeye amekuwa akiandika barua zenye kuzua migogoro, kuchafuana na kugombanisha wafanyakazi wenzake na afisa elimu wa wilaya hiyo Mathias Mkali.


Hatua ya Madiwani hao kumkataa Afisa elimu taaluma wa wilaya hiyo, imejitokeza hivi karibuni katika kikao cha Baraza hilo kilichoketi kwenye ukumbi wa Jumba la Maendeleo, uliopo mjini hapa.


Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani wilayani Mbinga ambaye alikuwa akiendesha kikao hicho, Winfrid Kapinga alisema wamekasirishwa na tuhuma hizo na kubaini kwa muda mrefu kuwa vitendo hivyo vinavyofanywa na Pilly, vinaweza kudumaza mikakati iliyowekwa ya kimaendeleo katika kukuza elimu wilayani humo.


Kapinga alifafanua kuwa Afisa elimu msingi wa wilaya hiyo Bw. Mkali alipohamia wilayani Mbinga mwaka 2011 aliweza kuinua kiwango cha taaluma kutoka asilimia 40 hadi kufikia asilimia 53.6 na kuifanya halmashauri hiyo kushika nafasi ya pili mkoani Ruvuma, kati ya wilaya tano zilizopo mkoani humo.


“Tumeamua kumkataa huyu mtu kutokana na matendo yake, ni vyema arejeshwe kwenye mamlaka yake ya uteuzi ili kuondoa migogoro hii ambayo imekuwa kero kubwa katika idara hii ya elimu”, alisema Kapinga.


Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa Mkali alipohamia wilayani Mbinga, aliweza kukabiliana na tatizo la watoto 1,744 wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK) kwa kuweka mikakati madhubuti ambayo ilishirikisha walimu wote mashuleni na kuifanya wilaya hiyo iweze kusonga mbele.


Pamoja na mambo mengine, Diwani wa kata ya Litembo Altho Hyera alipozungumza na Waandishi wa habari nje ya ukumbi wa mikutano, alisema hatua iliyochukuliwa na baraza hilo inapaswa kuungwa mkono huku akieleza kuwa Pilly amekuwa akiendeleza migogoro ya kuandika barua hizo, kwa kushirikiana na Katibu wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) tawi la Mbinga Samwel Mhaiki na kuufanya uongozi wa wilaya hiyo kushindwa kufanya kazi zake za kimaendeleo, kutokana na muda mwingi kuutumia kujibu tuhuma wanazoziandika katika barua hizo na kuzipeleka ngazi ya juu.


“Huyu Pilly muda mwingi yeye badala ya kufanya kazi anafikiria kuandika mabarua ya kuchafuana yasiyo na faida kwetu, kamati husika iliundwa kufuatilia jambo hili na imebaini kuwa hakuna ukweli wa mambo anayo andika na sisi tumeona hatufai………..aondoke”, alisema Hyera.


Naye Mwenyekiti wa Kamati ya elimu, afya na maji wilayani Mbinga ambaye ni Diwani wa kata ya Litumbandyosi, James Yaparama alieleza kuwa wamechoshwa na mambo yaliyofanywa na  afisa elimu taaluma wa wilaya hiyo hivyo hawaoni sababu ya kuendelea kukaa na mtu ambaye muda mwingi amekuwa akileta matatizo katika wilaya yao ambayo yakiendelea kufumbiwa macho huenda maendeleo katika sekta ya elimu yakarudi nyuma.


Hata hivyo alipoulizwa Pilly alieleza kuwa yeye tuhuma hizo anazisikia tu watu wakizungumza mitaani na bado hajapata barua rasmi ya kumuhamisha katika kituo chake cha kazi kutoka kwa mwajiri wake, huku akiongeza uamuzi uliochukuliwa na baraza hilo hautambui na ataendelea na kazi kama kawaida ambapo vilevile alipotafutwa kwa njia ya simu Katibu wa CWT tawi la Mbinga, Samwel Mhaiki ili aweze kujibia suala la kuhusishwa na tuhuma hizo, hakuweza kupatikana na simu yake ilikuwa imefungwa kwa muda mrefu.

No comments: