Wednesday, November 13, 2013

WAZAZI WILAYANI TUNDURU WATAKIWA KUWAJENGEA WATOTO WAO MALEZI BORA

Na Mwandishi wetu,
Tunduru.

WAZAZI na Walezi wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wameaswa kushirikiana na serikali kusimamia na kufuatilia   kwa karibu mienendo na maendeleo ya watoto wao hasa wa kike, ikiwa ni juhudi ya kuhakikisha  kuwa  watoto hao wanafanya  vizuri katika masomo yao na kujiletea maendeleo yao.

Ofisa mtendaji wa kata ya Mhuwesi  Shijabu Ngoronje alisema hayo wakati alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa Wadau wa elimu uliofanyika katika Kijiji cha Mhuwesi, ukiwa ni mwendelezo wa juhudi za mradi  wa usimamizi na utetezi wa haki ya mtoto wa kike kupata elimu .

Akifafanua taarifa hiyo Ngoronje alisema, ili kufanikisha adhima hiyo serikali imejipanga kutoa elimu kwa kuwaomba wazazi na walezi kujitoa kuchangia chakula  cha mchana kama kivutio kwa watoto wao na kuwafanya wapende masomo.


Kuhusu mila na desturi za makabila ya Wayao wilayani Tunduru, alisema kuwa tayari serikali imeunda kikosi kazi cha kuonana na viongozi wa mila, makungwi na manyakanga na kuwaomba wasaidie kuiwaelimisha juu ya utoaji wa elimu kwa watoto wa kike, na kuwafanya wapende masomo tofauti na sasa ambapo kundi hilo limekuwa likifundishwa kukabiliana na maisha ya ndoa hali inayosababisha kuwepo kwa matukio mengi ya ndoa za utotoni wakiwa shuleni.

Kuhusu wazazi wenye tabia za kutunza siri za watoto wao wakike baada ya kupewa mimba na wanaume kwa kisingizio cha kutaka kuwaozesha mapema alisema , serikali imejipanga kupambana nao kwa kuanza kuwachukulia hatua wazazi na watoto husika pamoja na manyakanga ambao wamekuwa wakitoa mafunzo mabaya wakati wa jando na unyago.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo Hakimu Kilowa   na Hussein Makoroboyi  katika maoni yao juu ya kinacho sababisha elimu kushuka wilayani humo, walidai kuwa Kipato duni cha akina mama ndio chanzo kikuu, ambapo mara nyingi ndio wamekuwa wakiachiwa jukumu la kutunza watoto wa kike .

Aidha wadau hao pia wakatumia nafasi hiyo kuwashukuru kuwapongeza  wafadhili wa mradi huoShirika la The Foundation for Civil Society (FCS) la Jijini Dar Es Salaam, kwamba mradi huo utaweza kuongeza msukumo kwa wazazi kuwahimiza watoto wao kwenda shule, pia kuwa apunguzia majukumu watoto wa kike na kuwaoza mapema kabla ya umri wao.

Shekhe mkuu wa Tunduru Alhaji Waziri Chilakwechi alipongeza  kuwepo kwa mradi huo, ambao alisema kuwa ni ukombozi kwa mtoto wa kike na utaweza kuongeza msukumo kwa wazazi kuwahimiza watoto wao kwenda shule, pia kuwapunguzia majukumu watoto wa kike na kuwaoza mapema kabla ya umri wao.

Awali akitoa taarifa ya mradi huo Meneja wa mradi wa shirika kiserikali la TUFAE Education Aids Trust, linalo simamia uhamasishaji huo John Nginga  alisema kuwa  mradi huo ulibuniwa kufuatia majibu mabaya ya utafiti uliofanywa na shirika hilo mwaka 2007 hadi 2010 na kubaini uwepo wa maendeleo mabaya ya elimu kwa mtoto wa kike wilayani humo, na kuchukua uamuzi wa kuhakikisha kuwa mtoto wa kike anapata  elimu kuanzia darasa la awali, elimu ya msingi, sekondari hadi Chuo Kikuu.

Nginga aliendelea kubainisha kuwa katika utafiti huo uliofanyika katika tarafa za Muhuwesi, Namasakata, Ligoma, Nandembo, Mlingoti Mashariki na  Mlingoti Magharibi wilayanbi Tunduru zilibainisha kuwapo kwa kundi kubwa la watoto wa kike waliopata mimba pamoja na kikwazo cha uelewa mdogo wa jamii juu ya sera ya elimu, haki ya mtoto wa kike kupata elimu na mila zilizopitwa na wakati.

Takwimu hizo zilifafanua kuwa katika kipindi cha mwaka 2007 hadi 2010 jumla ya waliotarajiwa kuandikishwa shule ni watoto wa kike 17,386, walioandikishwa ni 14,692 ambao ni sawa na asilimia 85.49%  na waliosajiliwa ni 13,411, na waliofanya mitihani wa kumaliza darasa la saba walikuwa 13,097 ambao ni sawa na asilimia 97.65%, huku kukiwa na anguko la watoto 314 ambao waliacha shule kwa sababu mbalimbali ikiwemo kupata mimba wakiwa shuleni pamoja na utoro.

 

No comments: