Tuesday, October 29, 2013

KERO YA UPATIKANAJI WA MAJI MJI WA SONGEA YAZIDI KUKERA WANANCHI

Mji wa Songea.























Na Muhidin Amri,
Songea.


WAKAZI wa Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wametakiwa kutumia maji kwa uangalifu kutokana na huduma hiyo kutolewa kwa mgao ambao unasababishwa na  ukosefu wa umeme wa uhakika katika Manispaa  hiyo, kutokana na mashine za kusukuma maji kwenda kwenye makazi ya watu kushindwa kufanya  kazi yake ipasavyo.


Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni, na afisa uhusiano wa Mamlaka ya maji safi na mazingira (SOUWASA) Neema  Chacha, alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini Songea.


Chacha alisema kufuatia tatizo  la umeme unaotolewa kwa mgao mjini Songea, mamlaka hiyo  hulazimika kutoa maji  kwa mgao pele umeme unapowaka na wao ndipo waweze kuwasha mashine zao.


Alisema kutumia jenereta pekee kufanya kazi za uendeshaji kuwa za gharama kubwa, na Mammlaka kupata hasara.


“Wananchi ni vyema nao wafahamu kuwa mji wa Songea umeingia kwenye tatizo kubwa la umeme, hivyo wanalazimika kutumia maji kwa uangalifu na  maji yanayototolewa sasa tunafahamu hayawezi kutosheleza watu wote   ikilinghanishwa na kipindi cha nyuma”, alisema Chacha.


Akizungumzia juu ya mgao huo ambao kwa sasa unaonekana kuwa kero kubwa kwa wakazi wa Songea, Chacha alibainisha kuwa, mgao huo unatekelezwa kwa maeneo yote ya mji huo, na hakuna eneo hata moja linalopendelewa hivyo ni muhimu kwao kuzingatia ratiba za upatikanaji wa maji ili kuwaondolewa usumbufu unaoweza kujitokeza.  


Aidha ametoa wito kwa wananchi, hususani wanaoishi  jirani na vyanzo vya maji kama katika milima ya Matogoro, Luhira, na Chemchem kuepuka tabia ya kuharibu vyanzo hivyo au kufanya shughuli  za kibinadamu  ikiwemo kulima au kuchungia mifugo katika maeneo hayo kwakufanya hivyo kunaweza kuleta madhara makubwa ikiwemo kukauka kwa vyanzo hivyo.

No comments: