Saturday, October 5, 2013

SERIKALI YATAKIWA KUENDELEA KUTOA ELIMU YA MAAMBUKIZI YA UKIMWI KWA WATU WALIO KATIKA MAKUNDI MAALUM

Aliyesimama ni Diwani wa viti maalum tarafa ya Mbinga mjini akitoa nasaha zake kwa washiriki wa semina ya watu wenye ulemavu(hawapo pichani)  Bi. Luciana Ndunguru, ambayo ilifanyika Mbinga mjini kwenye ukumbi wa Maktaba. Aliyevaa kofia ni Mwenyekiti wa Chama cha walemavu wilaya ya Mbinga, Martin Mbawala.

Washiriki wa semina ambao ni watu wenye ulemavu wa aina mbalimbali kutoka hapa wilayani Mbinga.


Na Mwandishi wetu,
Mbinga.

SERIKALI imeshauriwa kuendelea kuelimisha na kutoa mafunzo ya kujiepusha na maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI hususani kwa makundi maalum, ambayo kwa kiasi kikubwa yamekuwa yakitengwa katika jamii kwa namna moja au nyingine.

Kutengwa huko imeelezwa kuwa ni kuwanyima fursa katika uelewa wa mambo mbalimbali, jambo ambalo ni hatari kwa maendeleo ya kizazi cha sasa na kijacho.

Wito huo umetolewa leo kwenye semina ya siku moja, iliyolenga kuwafanya watu wenye ulemavu kutambua haki zao za msingi na sheria ya watu wenye ulemavu, ambayo imefanyika kwenye ukumbi wa Maktaba uliopo mjini hapa.   

Semina hiyo imefadhiliwa na shirika lisilo la kiserikali la ‘The foundation for civil Society’ kutoka jijini Dar es Salaam.

Sambamba na hilo serikali imetakiwa kuendelea kutilia mkazo na kufanyia utekelezaji mambo muhimu ikiwemo ujenzi rafiki wa miundombinu mashuleni, ofisi na hata kwa taasisi binafsi nazo zimeshauriwa kuzingatia hilo.

Aidha vifaa ya kusomea ambavyo vinahitajika mashuleni kwa kundi la watu wenye ulemavu, vinatakiwa viwepo ili kuliwezesha kundi hilo liweze kusoma kwa urahisi.

“Katika shule zetu hakuna vifaa maalum vya kusomea watu wenye ulemavu hususani kwa hawa wenzetu albino, viziwi na hata wasioona tunaiomba serikali izingatie hili kwa kuhakikisha miundombinu rafiki kwa walemavu inapatika mashuleni”, alisema Steven Matteso.

No comments: