Tuesday, October 29, 2013

KITUO CHA AFYA MCHOTEKA KINA HALI MBAYA, WANANCHI WAIOMBA SERIKALI KUNUSURU HALI HIYO

MKuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu.



















Na Dustan Ndunguru,
Songea.


KITUO cha afya cha Mchoteka kilichopo katika wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma kinakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo upungufu  wa watumishi, majengo na ukosefu wa  dawa na vifaa tiba huku wagonjwa wanaofika katika kituo hulazimika kutafuta huduma hiyo kwenye hospitali za misheni kwa gharama kubwa.


Mganga mkuu wa kituo hicho Dokta Tigrida Sanga alisema kituo hicho kinahudumia  wananchi wa kutoka  tarafa mbili ya Nalasi kwa wilaya ya Tunduru na Sasawala, na kwa upande wa wilaya ya Namtumbo na nchi jirani ya Msumbiji kutoka jimbo la Nampura.


Kituo hicho  kinatoa huduma ya chanjo kwa wajawazito na watoto, upimaji wa virusi vya UKIMWI na UKIMWI kwa wajawazito na kutoa elimu ya uzazi wa mpango, lakini wamekuwa wakikwama kutoa huduma hizo kutokana na kukabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo pia upungufu wa watumishi, majengo na vifaa tiba.


Alisema kwa sasa kituo kina watumishi wa sekta zote wapatao  saba kati ya 23 wanaohitajika, nyumba za watumishi zilizopo tatu kati ya 27, hakuna  jengo la maabara, hakuna jengo la upasuaji, jengo la ushauri nasaha na hawana  gari la kubeba wagonjwa, huku akidai hali hiyo inasababisha  watumishi wa kituo hicho  kufanyakazi katika mazingira mgumu.


Katika kuthamini mchango wa wananchi na serikali yao, wizara kupitia halmashauri yao imeweza kutoa video kwa ajili ya kupeleka ujumbe kwa wananchi juu ya kuwapatia elimu ya kujikinga na maambukizo ya magonjwa ya zinaa na UKIMWI, lakini alidai video hivyo vimekosa mikanda na hivyo wananchi wamekuwa wakiikosa elimu hiyo.


Alisema pamoja na kukabiliwa na changamoto nyingi za kiutendaji bado kituo hicho  kimekosa huduma ya nishati ya  umeme wa jua (Solar) kutokana na kuharibika na taarifa wameweza kutoa kwa idara husika, lakini alidai hakuna kinachoendelea na kwamba kutokana na kukosekana kwa nishati hiyo wagonjwa wanaolazwa kituoni hapo hulazimika kutumia taa za chemli kumulikia wakati wa usiku.

No comments: