Saturday, October 5, 2013

NGAGA AWAHIMIZA VIJANA KUJIKITA KATIKA SHUGHULI ZA KIMAENDELEO

Mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga(aliyevaa suti nyeusi) akikagua gwaride  wakati wa kufunga mafunzo ya vijana zaidi ya 1000  katika kikosi cha 842 Kj Mlale JKT, kushoto ni mkuu wa gwaride Hilo Capt. Gerald William Rwenyagira. (Picha na Muhidin Amri)



Na Muhidin Amri,
Ruvuma.

VIJANA nchini wamehimizwa kujikita zaidi katika shughuli za maendeleo na kujiepusha kushiriki katika mambo yasiokuwa na manufaa kwao, ambayo yanaweza kuwaharibia mustakabali wa maisha yao ikiwemo  kushiriki kwenye maandamano ya vyama vya siasa ambayo mara nyingi yamekuwa na dhamira ya kuanzisha chuki na uhasama, kati ya serikali na wananchi.


Hayo yamesemwa  hivi karibuni wilayani Songea na Mkuu wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Senyi Ngaga, wakati akifunga mafunzo ya miezi mitatu kwa vijana wa kujitolea  Operesheni miaka 50 ya JKT na miaka 50 ya vijana kwa mujibu wa sheria, Julai hadi Septemba mwaka huu katika kikosi cha 842 KJ Mlale JKT mkoani humo.


Mkuu huyo wa wilaya alisema vijana wana nafasi kubwa ya kulifanyia mambo mazuri taifa hili, tofauti na wao wanavyofikiria lakini inaonesha kwamba tatizo kubwa walilonalo ni kutojitambua ndiyo maana wanadiriki kushiriki katika mambo ambayo ni tofauti na umri walionao na hata kujikuta wakipoteza muda wao mwingi, katika vitu ambavyo  vinavyowapotezea muda.


Alikemea tabia iliyoanzishwa na baadhi ya vyama vya siasa kuwahamasisha vijana kuanzisha fujo, badala ya kuwahimiza kushiriki katika kazi za ujenzi wa taifa hili licha ya kufahamu kuwa vijana ndiyo taifa la kesho na hakuna nchi yeyote duniani iliyopiga hatua za kimaendeleo bila ya mchango wa vijana wake.


Ngaga alisema tabia inayofanywa na viongozi wa vyama hivyo haifai na inatakiwa kukemewa na kukomeshwa, lakini hayo yote yanawezekana iwapo tu vijana wenyewe  watakataa kutumiwa na watu hao kwa masalahi yao binafsi na kusisitiza kuwa taifa lolote haliwezi kupiga hatua mbele, kwa  watu wake kushiriki maandamano au kufanya fujo.  


Aliongeza kuwa lengo la Serikali kurudisha mafunzo ya JKT ni kutaka kuwakusanya vijana kutoka  sehemu mbalimbali nchini, ili kuwafundisha uzalendo wa nchi yao na wengine  watakao bahatika kupata ajira serikalini, wawe viongozi bora watakaowasaidia watanzania wenzao katika kujenga nchi imara na yenye mshikamano thabiti.


Alibainisha kuwa vijana wengi ambao kwa sasa ni viongozi katika idara za serikali na hata mashirika ya umma waliopitia mafunzo hayo wamekuwa viongozi wazuri katika taifa hili, ukilinganisha na wale waliopata nafasi hiyo bila ya kupitia mafunzo hayo na matokeo yake kila siku wamekuwa watu wa kulalamika badala ya kutafuta njia ya kuwasaidia wenzao, kutafuta suluhu ya kero au matatizo yanayowakabili.


Katika mafunzo hayo jumla ya vijana 1123 kati yao wavulana 890 na wasichana 238 walihitimu mafunzo ya awali ya kijeshi katika kikosi hicho, ambapo pia kwa wale wa kujitolea wataendelea na kozi za fani mbalimbali za ujasiliamali.




No comments: