Saturday, October 26, 2013

HALMASHAURI YA WILAYA YA MBINGA LAWAMANI KWA KUTELEKEZA BUSTANI MAMA ZA KUZALISHIA MICHE YA KAHAWA, MENEJA ASEMA TATIZO HILO LIKIENDELEA KUFUMBIWA MACHO UCHUMI WA WILAYA HIYO HUENDA UKADOROLA

Meneja wa Kanda ya Kusini Godbless Shao, alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya Bustani mama za kuzalishia miche ya kahawa zilivyotelekezwa wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma. (Picha na Kassian Nyandindi)




Na Kassian Nyandindi,
Songea.

BUSTANI Mama za kuzalishia miche ya kahawa, wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma zipo katika hali mbaya na huenda uzalishaji wa miche hiyo ukashindwa kuendelea, kutokana na Halmashauri ya wilaya hiyo kuzitelekeza bustani hizo kwa kutosimamia na kufuata taratibu husika.

Sambamba na hilo uongozi husika wa wilaya hiyo umeshushiwa shutuma nzito juu ya uzembe huo, kwa kile kilichoelezwa kuwa licha ya Taasisi ya Utafiti wa zao la Kahawa Tanzania (TaCRI) – Ugano Kanda ya kusini, kutoa ushauri wa mara kwa mara juu ya kuendeleza bustani hizo hali ambayo hivi sasa imekuwa tete na hakuna utekelezaji unaofanyika.

Meneja wa Kanda ya Kusini Godbless Shao, alisema hayo alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari mjini hapa ambapo alitahadharisha kuwa, endapo suala hilo litaendelea kupuuzwa huenda uchumi wa wilaya ya Mbinga ukashuka kwa kasi, kutokana na tegemeo kubwa la kukua kwa uchumi wilayani humo hutegemea zao la kahawa.

Shao alieleza kuwa bustani hizo ambazo zilianzishwa na TaCRI baadaye kukabidhiwa halmashauri hiyo kwa ajili ya kusimamia na kuendeleza uzalishaji wa miche ya kahawa, hivi sasa zinaelekea kufa kutokana na kuwepo usimamizi duni wa wataalamu husika.

“Ni jambo ambalo kwa kweli tusipokuwa makini na tukafanyia mzaha hizi bustani kwa sasa zina hali mbaya, baadhi yake zina kufa licha ya TaCRI kutoa mchango wake mkubwa, nina imani hapo baadaye tusipo zingatia kanuni za uzalishaji bora wa kahawa uchumi wa wilaya hii huenda ukashuka na hili linasikitisha sana,

“TaCRI tayari kazi kubwa tumeifanya kwa kujenga bustani nyingi za kuzalishia miche, lakini sasa zina hali mbaya kutokana na Halmashauri ya wilaya ya Mbinga kutoshughulikia bustani hizi”, alisema Shao.

Hata hivyo Meneja huyo kwa upande wa Wakulima wanaojishughulisha na uzalishaji wa kahawa wilayani humo, aliwataka kuendelea kuzingatia kanuni bora za kilimo ikiwemo matumizi bora ya mitambo ya kukobolea kahawa mbivu vijijini.

No comments: