Tuesday, October 8, 2013

ASKARI MGAMBO WANUSURIKA KUUAWA KATIKA VURUGU WILAYANI MBINGA

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
 
VURUGU zilizodumu kwa masaa matano zimejitokeza katika kijiji cha Lipilipili kata ya Mpepai wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, na askari wa nne wa Jeshi la mgambo wilayani humo akiwemo ofisa mtendaji wa kijiji hicho, wamenusurika kuuawa kufuatia wananchi wenye hasira kali, kuwashambulia wakiwa kwenye majukumu yao ya kazi.
 
Hali hiyo imejitokeza majira ya saa 1:30 asubuhi, Oktoba 7 mwaka huu ambapo mgambo na mtendaji huyo walikwenda kijijini hapo kutekeleza azimio la kikao cha kamati ya maendeleo ya kata hiyo, ambacho kilifikia uamuzi wa waliokataa katani humo kuchangia shughuli za ujenzi wa maabara na bweni la kulala wanafunzi katika shule ya sekondari Dokta Shein, wakamatwe na kuchangia kila mmoja shilingi 25,000 ya mchango husika.
 
Akizungumza na waandishi wa habari, ofisa mtendaji wa kata ya Mpepai Anssila Kumburu alisema, katika kikao cha kamati hiyo kilichoketi kijiji cha Luhangai Septemba 27 mwaka huu, Mwenyekiti wa kamati ambaye ni Diwani wa kata hiyo Francis Nchimbi ndiyo yeye aliyetangaza uamuzi huo wa kuleta mgambo, kwa ajili ya kusaidia kuwasaka wale wote  waliokataa kuchangia miradi hiyo ya maendeleo.
 
Kumburu alisema Septemba 30 mwaka huu ndipo mgambo hao walianza kutekeleza jukumu hiyo kwa kushirikikiana na maofisa watendaji wa vijiji vya kata ya Mpepai, kupita kwa kila kaya kukusanya michango husika ambapo kati ya vijiji vitano vya kata hiyo, vijiji vinne walivyopita hapakuwa na tatizo lolote lile wananchi wake waliitikia wito huo kwa kutoa michango waliyoelekezwa.
 
Kufikia Oktoba 7 mwaka huu wakiwa kitongoji cha Mtukula kijiji cha Lipilipili katani humo, Mgambo tisa wakiwa na ofisa mtendaji wa kijiji hicho Petro Mayowa walishambuliwa na wananchi kwa kupigwa seheme mbalimbali za mwili kwa kutumia silaha za jadi.
 
Alifafanua kuwa baada ya tukio hilo wananchi hao walimchukua Ofisa mtendaji wa kijiji hicho na kumpeleka ofisini kwake, ambako walimwingiza ndani na kumfungia huku wakiwa tayari wamemjeruhi vibaya maeneo ya kichwani huku akivuja damu kwa wingi.
 
“Kutokana na tukio hili la kufungiwa ndani, wasamaria wema walijitokeza baada ya masaa mawili na kuvunja mlango wa ofisi hiyo wakati majeruhi alipokuwa akipaza sauti za kuomba msaada”, alisema Kumburu.
 
Kufuatia tukio hilo ambalo ofisa mtendaji huyo aliripoti polisi akiwa na majeruhi ambao ni mgambo, Loy Mbunda, Joseph Alli, Kanisius Ngonyani, Agness Mwilafi na mtendaji huyo wa kijiji ambapo baadaye walifikishwa katika hospitali ya wilaya ya Mbinga kwa ajili ya matibabu.
 
Kwa mujibu wa Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo Robert Elisha, pamoja na kukiri kupokea majeruhi hao alisema walipatiwa matibabu ambapo mtendaji wa kijiji cha Lipilipili Petro Mayowa, ambaye aliumizwa vibaya  alishonwa kichwani na hao wenzake ambao waliumizwa sehemu mbalimbali za miili yao walipatiwa matibabu na kuruhusiwa.
 
Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma, limethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo Kamanda wa polisi wa mkoa huo Deusdedit Nsimeki alisema baada ya polisi kupata taarifa ya tukio hilo walikwenda huko na kufanikiwa kuwakamata wanakijiji wa nane ambao wanadaiwa kuhusika na vurugu hizo.
 
Nsimeki aliwataja watuhumiwa kuwa ni Bonventure Kapinga, John Nchimbi, Kondrad Haulle, Willson Kapinga, Thomas Kapinga, Maiko Kapinga, Zackaria Ndunguru na Amos Ndunguru.
 
Alieleza kuwa wanakijiji hao walitumia silaha aina ya Panga, magongo na fimbo za mianzi kuwapiga mgambo hao na kwamba polisi wanaendelea kuwahoji na upelelezi utakapokamilika watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zitakazowakabili.

No comments: