Tuesday, October 29, 2013

UKOMBOZI SACCOS JIMBO LA SONGEA YAJIVUNIA MAFANIKIO YAKE

Rais Jakaya Kikwete.























Na Dustan Ndunguru,
Songea.

CHAMA cha akiba na mikopo cha Ukombozi Jimbo la Songea (SACCOS) kilichopo katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, kimekopesha wanachama wake shilingi bilioni 2.2 katika kipindi cha miaka saba tangu kuanzishwa kwake.


Meneja wa SACCOS hiyo Rainer Ngatunga alisema kuwa fedha hizo zilizokopeshwa ni kutokana na akiba za wanachama, na sasa chama kina wanachama 1104.


Ngatunga alisema kuwa kati ya fedha hizo shilingi bilioni 1.6 zimekwisha rejeshwa huku akiwataka wanachama wake, watumie fedha wanazokopeshwa kwa malengo yaliyokusudiwa sambamba na kujenga tabia ya kurejesha mikopo wanayokopa kwa wakati.  


“Kipindi hiki ambacho msimu wa kilimo unatarajia kuanza wanachama wanapaswa kupeleka maombi ya mkopo wa kilimo na ada kabla ya Novemba mosi mwaka huu, lakini pia kila mwanachama ahakikishe anaanzisha miradi ya kiuchumi ili fedha anazokopeshwa aweze kuelekeza katika eneo husika na kuweza kukuza mtaji wake”, alisema.


Alisema lengo la chama ni kuona kila mwanachama ananufaika na mikopo inayotolewa ambapo mpaka sasa wengi wao wanaendelea vizuri na shughuli mbalimbali.  


Ngatunga alisema wanajivunia kitendo chao cha kutotegemea kukopa katika taasisi zingine za kifedha hususani benki, kwani kutokana na hali hiyo wamekuwa wakiepuka riba kubwa inayotozwa na benki baada ya kukopa hivyo katika kuepukana na hilo wanachama wahakikishe wanaendelea kuweka akiba zao katika SACCOS yao.

Aliishukuru serikali kwa kuendelea kuhamasisha wananchi wake kuanzisha vyama vya akiba na mikopo na vikundi vya ujasiriamali, jambo ambalo ni msaada mkubwa kwa wananchi ambao kimsingi walikuwa wakiogopa kukopa benki kutokana na riba kuwa kubwa.

No comments: