Thursday, October 17, 2013

MBUNGE KAYOMBO ASIKITISHWA NA HATUA YA SERIKALI KUPIGA MABOMU WANANCHI, ASEMA YUPO TAYARI KUFIKISHA MADAI YAO KWA MWANASHERIA ILI HAKI ZAO ZIWEZE KUPATIKANA

Mtambo ukiendelea na uchimbaji wa Makaa ya mawe katika mgodi wa Ngaka, huko katika kijiji cha Ntunduaro kata Ruanda wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma.



Na Kassian Nyandindi,
Ruvuma.


HATUA iliyochukuliwa na Serikali kupiga mabomu kwa ajili ya kuwatawanya wananchi waliokuwa wakiandamana kwa amani katika kijiji cha Ntunduaro kata ya Ruanda mkoani Ruvuma, Mbunge wa jimbo la Mbinga Gaudence Kayombo, ameshusha lawama nzito na kusema hajafurahishwa na kitendo hicho.


Gaudence Kayombo amesema, nguvu iliyotumika ni kubwa na hapakuwa na sababu kwa serikali kufanya hivyo, kutokana na wananchi wa kijiji hicho madai yao wanayoyadai ni ya msingi na muda mrefu sasa, umepita hawajatekelezewa.


Mbunge huyo alisema hayo alipokuwa akihojiwa na Mwandishi wa habari hizi juu ya wananchi hao wamekuwa wakilalamika kwa muda mrefu, wakidai fidia zao katika eneo ambalo waliondolewa kwa ajili ya kupisha shughuli za mgodi wa Ngaka, ambapo huchimbwa makaa ya mawe.


”Kule imetumika nguvu kubwa ya polisi kupiga mabomu wale wananchi, hapakuwa na sababu badala yake serikali itoke mbele na ieleze hawa wanaodai fidia zao lini watalipwa”, alisema Kayombo.


Alisema kuwa kuna baadhi yao wengine hawajalipwa kabisa na wananchi karibu 400 ambao awali walilipwa fidia zao, ilionekana fedha walizolipwa ni kidogo hivyo nao walipewa ahadi ya kuongezewa malipo mengine, jambo ambalo hadi leo hii halijatekelezwa.


Kayombo alisisitiza akisema ni vyema serikali itimize wajibu wake, kwa kuelimisha wananchi na sio kutumia nguvu kubwa kwa kuwapiga mabomu ambayo yanaathiri jamii.


Alifafanua kuwa endapo tatizo hili litaonekana kuendelea kuwa sugu, yeye kwa nafasi yake yupo tayari kuwasaidia wananchi wa kijiji hicho kufikisha madai yao kwa Mwanasheria na hatimaye yapelekwe Mahakamani ili haki iweze kupatikana.


“Nipo tayari kuwasaidia hawa wananchi kwa kuwatafutia Wanasheria ambao wataweza kusimamia jambo hili kwa umakini katika kusaidia kudai haki zao, ili ziweze kupatikana”, alisema.


Mbunge Kayombo alisema, Wananchi wa kijiji cha Ntunduaro wanasikitishwa pia na hali ya mazingira ilivyokuwa mbaya kwao ambapo vumbi la barabarani, wakati wa usafirishaji wa makaa ya mawe limekuwa likiwaathiri afya zao hivyo, wanaiomba mamlaka husika kumshauri mmiliki wa mgodi huo kuweka mazingira katika hali nzuri.


Pia alisema Mwekezaji wa mgodi huo wa Ngaka alitoa ahadi ya kuwajengea miundombinu ya maji wananchi hao, lakini utekelezaji wa ahadi hiyo haujafanyika hadi sasa ndio maana kumekuwa na malalamiko ya hapa na pale.


“Hawa wananchi leo hawana maji ya uhakika katika kuendeshea maisha yao, hivi hapa kweli inaingia akilini kwa binadamu ambaye ni kiumbe hai unaweza kuishi bila kupata maji safi na salama”,? alihoji Kayombo.


Mto Nyamabeva uliopo katika kijiji hicho ambao ndio tegemeo kubwa, maji yake yamechafuliwa na wawekezaji hao kutokana na vumbi la sumu ya mkaa wa mawe.


Matatizo na dhuluma iliyopo yanasababishwa na viongozi wa serikali, huku baadhi ya wananchi wakiteseka na kuugua magonjwa mbalimbali kutokana na  kunywa maji yenye chembechembe ya sumu ya madini ya makaa ya mawe, yanayochimbwa katika mgodi huo.


Hata hivyo mradi huo wa makaa ya mawe unamilikiwa na kampuni ya ubia ya Tancoal Energy, ambayo asilimia 30 ya hisa zake zinamilikiwa na serikali kupitia shirika la maendeleo la Taifa NDC, na asilimia 70 ya hisa zinamilikiwa na mwekezaji wa kampuni ya Intra Energy.

No comments: