Tuesday, October 29, 2013

MFANYABIASHARA MWENYE ASILI YA KIARABU APANDISHWA KIZIMBANI KATIKA MAHAKAMA YA WILAYA YA MBINGA KWA KOSA LA KUTUNZA SILAHA KWA UZEMBE

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman.


























Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

MFANYABIASHARA mmoja ambaye ni raia mwenye asili ya kiarabu amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, kwa kosa la kutunza silaha kwa uzembe kitendo ambacho ni hatari katika jamii.

Kwa mujibu wa Mwendesha mashataka wa polisi Inspekta Mwamba alimtaja raia huyo kuwa ni Karama Abdallah Karama (37) ambaye anaishi Mbinga mjini, alitenda kosa hilo Oktoba 10 mwaka huu majira ya saa 5:30 asubuhi.

Mwendesha mashataka huyo alidai mbele ya Hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama wilaya hiyo Geofrey Mhini kuwa, silaha hiyo ni Pisto aina ya Bereta yenye namba za usajili H 30436Y.

Alisema  raia huyo alikamatwa na maofisa wa Jeshi (JWTZ) ambao walikuwa kwenye oparesheni “Okoa Maliasili”, ambapo walipobaini uzembe huo walimuamuru mfanyabiashara huyo aitoe silaha ambayo ilikutwa ikiwa imehifadhiwa katika eneo la kituo cha mafuta cha Oil Com kilichopo mjini hapa, ikiwa katika mazingira ya hatari.

Maofisa hao wa Jeshi wakati huo walikuwa wakimfanyia upekuzi Bw. Karama, baada ya kuihisiwa anafanya biashara ya kusafirisha Nyara za serikali pasipo kibali maalum ndipo walipobaini kuwepo na tatizo la uzembe wa utunzaji wa silaha, ambayo anaimiliki kisheria.

Ilidaiwa Mahakamani hapo kuwa wakati maofisa hao wa Jeshi wakiwa katika eneo hilo la tukio cha kushangaza mshtakiwa huyo alipokuwa chini ya ulinzi huku akiambiwa aitoe silaha, yeye alikuwa akikataa huku akimwambia mfanyakazi wake wa chini aliyekuwa katika eneo hilo la kituo cha mafuta aitwaye Athumani Said, kwamba akaichukue ipo ndani ofisini kwake ambapo mfanyakazi huyo alikataa na kumtaka aende akaichukue mwenyewe.

Inspekta Mwamba alisema baada ya majibizano ya muda mrefu ndipo maofisa wa JWTZ kikosi cha Okoa Maliasili, walichukua jukumu la kumuamuru mshtakiwa aende akaichukue yeye mwenyewe na baadaye alitii amri na kwenda kuichukua, ndipo waliikuta ikiwa kwenye mkoba wa plastiki katika mazingira ya hatari.

Silaha hiyo ilikutwa na risasi 23 zilizokuwa na magazine mbili ambapo mshtakiwa huyo alianza kuimiliki kisheria mwaka 2008.

Hata hivyo kesi hiyo itakuja kwa ajili ya kusikilizwa tena Novemba 11 mwaka huu na kwamba mshtakiwa yupo nje kwa dhamana.

No comments: