Tuesday, October 29, 2013

WAZAZI NA WALEZI WATAKIWA KUFUATILIA MIENENDO YA WATOTO KWA KUHAKIKISHA WANAZINGATIA MASOMO

Waziri wa elimu na mafunzo ya ufundi, Shukuru Kawambwa.


























Na Dustan Ndunguru,
Songea.

SERIKALI mkoani Ruvuma imewataka  wazazi na walezi kuhakikisha wanafuatilia kwa ukaribu mienendo ya watoto wao, ili wasijiingize katika vitendo viovu ambavyo vinawafanya washindwe kuendelea na masomo yao.


Mkuu wa mkoa huo Said Mwambungu alisema baadhi ya wazazi na walezi wamekuwa na kawaida ya kutofuatilia watoto wao, jambo ambalo halipaswi kuendelea kuvumiliwa, kutokana na ukweli kuwa madhara yake ni makubwa pale wanapojiingiza katika matendo yasiyokubalika mbele ya jamii.


Mwambungu alisema alisema hayo alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi, huku akisisitiza kila mtoto anayefikisha umri wa kuanza shule anapaswa kuandikishwa na awapo shuleni maendeleo yake yanapaswa kufuatiliwa kwa ukaribu, kwa ushirikiano kati ya walimu na wazazi au walezi.


Alisema walio wengi wanadhani kwamba mwalimu pekee ndiye mwenye jukumu la kufuatilia maendeleo ya mwanafunzi,  wakati inafahamika wazi kuwa yeye anakuwa nao tu pindi wawapo shuleni lakini mara wakishatoka na kwenda majumbani kwao, wazazi ndio wanapaswa kubeba jukumu hilo.


Alisema wakati huu ambao wanafunzi waliohitimu elimu ya msingi wanasubiri majibu yao hawana budi kuwa makini, kwani baadhi ya wazazi au walezi wao wamekuwa na kawaida ya kutowatendea haki watoto wa kike ambapo wakati mwingine hukimbilia kuwaozesha, kitendo ambacho kamwe hakiwezi kukubalika katika jamii.

Mwambungu alisema watoto wa kike wanahaki sawa kama ilivyo kwa watoto wa kiume, hivyo jitihada zifanyike ili kuhakikisha hawarubuniwi na watu ambao hawawatakii mema na wale ambao watabainika kuendekeza vitendo hivyo, watachukuliwa hatua za kisheria.

No comments: