Saturday, October 19, 2013

WAZIRI MKUU AOMBWA KUIOKOA NFRA, NI BAADA YA KUDAIWA KUISHIWA FEDHA ZA KUNUNULIA MAHINDI

Waziri Mkuu Mizengo Pinda.

 

 

 

 

 

 

 

 


Na Mwandishi Wetu,
Makambako.

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda, ameombwa na wakulima wa mahindi katika mikoa ya Iringa, Ruvuma na Njombe, kuisaidia Wakala wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), kupata fedha za kuendelea kununua mahindi kwenye vituo vyake.

Wakulima hao wamedai kufikia hatua hiyo, baada ya kutangaziwa na NFRA kusitishwa kwa zoezi lililokuwa likiendelea kwa miezi miwili sasa ya kununua mahindi kutoka kwao, huku wakiishauri ofisi yake kuangalia uwezekano wa kumsaidia mkulima.

Wakizungumza na gazeti hili, wakulima wao wamedai kusikitishwa na uamuzi huo na kudai kuwa unaweza kuathiri mfumo wa kilimo kwa vile wao waliamini ushawishi wa serikali katika kuhimiza vijana kuingia katika sekta hiyo.

Wakulima hao wamedai kuwa wanaimani na ofisi ya Waziri Mkuu Pinda pekee, kuweza kuwasaidia kwa kuchukua uamuzi mgumu wa kuipatia NFRA fedha za kununua kiasi cha tani 200,000 zilizobaki kwa wakulima.
Mkulima wa Kijiji cha Mawengi, wilaya ya Ludewa, Agnes Mkinga, alisema baada ya tangazo la NFRA kusitisha ununuzi wa mahindi yao, watu wengi wameanza kupoteza imani na serikali.

“Hivi inakuwaje kwa serikali kushawishi wananchi kushiriki katika kilimo, alafu inatuachia njiani bila kutusaidia kuyanunua mahindi haya,” alisema Agnes.

Mkulima huyo alisema mazingira ya soko la misimu yote la NFRA ndilo limewafanya wananchi wengi kuongeza maeneo ya kilimo huku wakiingia gharama za mikopo kwa ajili ya kununulia pembejeo ili kuwa na mavuno bora.

“Tumefanya kazi kubwa mashambani, tumeambia kuwa serikali iliiagiza NFRA kununua tani 200,000 tu kwa maeneo yote ya nchi, lakini tunasema wazi kuwa kiasi hicho ni kidogo sana kwani ni sawa na mahitaji ya wakulima wa wilaya ya Ludewa pekee,” alisema Agnes.

Alisema mwaka jana baada ya msimu wa ununuzi kusitishwa kwa NFRA kukosa fedha, mahindi ya wananchi wengi yaliharibika kwa kukosa maeneo maalum kwa ajili ya uhifadhi, huku wengine wakiamua kuyatumia kwa kupika pombe za asili.

“Hayo sio matumizi bora na yenye tija na kamwe hayakidhi haja ya kilimo, kwani mwaka jana mahindi mengi yaliozoea kwenye nyumba za wakulima, na kama serikali haitaongeza fedha moyo wa watu kushiriki katika kilimo utapotea,” alisema Hilda Mgaya, wa kijiji cha Lugumbiro.

Mganya aliongeza na kusema kwamba wakulima wamefurahishwa na bei za mwaka huu zilizotangazwa na NFRA, lakini wameshindwa kuelewa maamuzi ya kusitisha ununuzi yamechukulia na kiongzi gani ili jamii yao ione umuhimu wa kumfuata.

“Tunahitaji kujua nini kimetokea na nani amechukua uamuzi huo, hivyo tunamuomba Mheshimiwa Waziri Mkuu Pinda, kuingilia kati suala hilo kwa nia ya kutusaidia sisi wakulima na hasa wa wilaya ya Ludewa ambao tupo pembezoni,” alisema Mgaya.

Kwa upande wake mkulima Osward Msafiri, wa kijiji cha Lufumbu, aliishauri serikali kufanya maamuzi ya haraka ya kutengua mpango wa NFRA na kutoa fedha ili zoezi la ununuzi wa mahindi liweze kuendelea.

Msafiri alisema kwamba serikali na hasa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, inapaswa kutambua wazi hali ngumu ya maisha ya vijana waliopo vijijini na ambao hivi sasa wameamua kutumia nguvu zao kuwekeza katika kilimo.

“Kukosekana kwa soko la uhakika tena la serikali kupitia NFRA ni sawa na kutaka kumvurugia malengo na kumsababishia msomo wa mawazo na kumkoroga kisaikolojia kijana ambaye sasa ni nguvu kazi katika uzalishaji,” alisema Msemwa.

Mkulima wa Mliyayoyo wilaya ya Songea Vijijini, ambaye pia ni Mwenyekiti wa umoja wa wakulima wa mahindi mkoani Ruvuma Damas Komba, alisema baada ya NFRA kusitisha ununuzi wa mahindi, serikali isitarajie mwamko wa wananchi katika sekta ya kilimo.

“Unajua huku wananchi wa wilaya za Mbinga, Songea na Namtumbo, wamefanya kazi kubwa sana, lakini pia wamepata mavuno mengi ya mahindi sasa kuambiwa NFRA haina fedha za kununua mahindi ni sawa na kutangaza janga,” alisema Komba.

Komba aliongeza kusema kwamba wakulima wamejitahidi kufanya kazi hiyo ya uzalishaji kwa kuweka baadhi ya mali zao rehani ili kufikia malengo ya uzalishaji, sasa kuambiwa kuwa NFRA haina fedha ni kutaka kumuongezea machungu ya maisha mkulima.

Mwenyekiti wa Muungano wa vikundi vya wakulima wa mahindi mkoa wa Iringa, Yohanes Mhanga, alisema wakulima wamesikitishwa na uamuzi wa NFRA kusitisha ununuzi wakati wananchi bado wakiwa na shehena kubwa.

Mhanga alisema ikiwa serikali haitakubali kuongeza fedha ili kuipa nguvu na uwezo NFRA kununua kiasi kikubwa cha mahindi hayo, wakulima wengi hawataona umuhimu wa kuendelea na kilimo cha mahindi, badala yake watalima nyanya na vitunguu.

Alimuomba Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Mhandisi Christopher Chiza, kuangalia jinsi ya kumsaidia mkulima na hasa wa kijijini, akisema kuwaachia kiasi hicho cha mahindi wakati walitarajia kuiuzia NFRA ni kuikwaza sekta.

Maafisa wa NFRA walizungumza na mwandishi wa habari hizi, walikiri kufikiwa kwa uamuzi wa kusitisha na wala sio kufunga kabisa vituo vya ununuzi, baada ya malengo ya kununua kiasi cha tani 200,000 nchini kufikiwa.

Hata hivyo, walidai kwamba ikiwa serikali itaona inafaa kuchukua hatua za kuwasaidia wakulima kwa kutoa amri ya kuendelea kununua zaidi, NFRA haina tatizo la kufanya hivyo.

No comments: