|
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Mbinga, Christantus Mbunda. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
HATIMAYE Diwani wa kata ya Kitanda, Zeno Mbunda Halmashauri
ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma amejikuta akiendelea kuwa katika wakati mgumu
baada ya kusimama mbele ya kikao maalumu na kuwaomba radhi baadhi ya Wananchi
na Wajumbe wa Baraza la maendeleo la kata hiyo, huku akikiri kwamba tuhuma
anazotuhumiwa kufanya ubadhirifu wa mali na fedha za wananchi hao kuwa ni za
kweli.
|
Zeno Mbunda, Diwani kata ya Kitanda. |
Pamoja na diwani huyo kukubali makosa hayo mbele ya kikao
hicho kilichofanyika Juni 17 mwaka huu kwenye Ofisi za makao makuu ya kata ya
Kitanda, aidha alieleza kuwa ifikapo Julai Mosi mwaka huu atakuwa amelipa mali
na fedha zote ambazo anadaiwa kutofikisha katani humo.
Radhi hiyo ambayo alikuwa akiiomba mbele ya ushuhuda wa viongozi
wa CCM wilaya ya Mbinga, akiwemo na Mwenyekiti wa Chama hicho Christantus
Mbunda ambaye alikuwa akiongoza kikao hicho.
Licha ya kuwaomba radhi bado Wajumbe wa baraza hilo la
maendeleo la kata walionekana kutoridhishwa na hali hiyo huku wengine wakisema
kuwa hawawezi kuchukua hatua ya kumsamehe, kwani ni mapema mno mpaka pale
atakaporejesha mali na fedha za wakulima wa kahawa anazotuhumiwa kuzitafuna kwa manufaa yake binafsi.
“Hatuwezi kuchukua hatua ya kumsamehe mpaka pia tupate majibu
ya hatua zilizochukuliwa kutoka Ofisi ya Mkuu wa wilaya, ambako malalamiko haya
tuliyapeleka kwa njia ya maandishi na bado hatujajibiwa mpaka sasa”, alisema
Mwenyekiti wa kata ya Kitanda Philibert Mkolwe.