Friday, October 24, 2014

ASKARI WA USALAMA BARABARANI MBINGA ASWEKWA MAHABUSU KWA KUMJERUHI DEREVA WA PIKIPIKI




Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

JESHI la Polisi wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, limeingia katika kashfa mpya kufuatia askari wake wa usalama barabarani kumjeruhi mwendesha pikipiki kwa kumchoma na kitu chenye ncha kali kichwani, na kumsababishia jeraha ambalo lilisababisha dereva huyo kutokwa na damu nyingi.

Tukio hilo lilitokea Oktoba 20 mwaka huu majira ya mchana, eneo la stendi ya magari ya abiria mjini hapa, ambapo askari huyo anayejulikana kwa jina la Msafiri Kilango, ndiye aliyefanya kitendo hicho kwa kumchoma kichwani dereva wa pikipiki aitwaye Erick Shonga.

Kufuatia tukio hilo hali ilibadilika mjini hapa ambapo kundi la waendesha pikipiki liliandamana kuelekea kituo kikuu cha polisi cha wilaya hiyo, kwa lengo la kupinga kitendo alichofanyiwa mwenzao.

Walipofika kituoni hapo walieleza malalamiko yao wakisema kuwa askari wa usalama barabarani wilayani hapa, wamekuwa na mazoea ya kuwanyanyasa mara kwa mara waendesha pikipiki hivyo wamechoshwa na hali hiyo.

“Sisi tumechoshwa na unyanyasaji huu ambao tunafanyiwa na hawa askari, muda mwingi wakitukamata wanatupiga faini wanachukua hela zetu halafu stakabadhi ya malipo halali hatupewi”, alisema Thito Mhina mmoja kati ya madereva hao wa pikipiki.

Aliyechomwa atoa ushuhuda:

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi dereva wa pikipiki aliyejeruhiwa Erick Shonga alisema, amepatiwa matibabu katika hospitali ya wilaya hiyo ambapo ameshonwa nyuzi tatu kichwani katika eneo ambalo alichomwa na kitu chenye ncha kali kichwani.

“Huyo askari amekuwa na mazoea ya kunisimamisha barabarani hata wakati mwingine nisipokuwa na makosa na ananiambia nimpe hela, siku ananikamata na kunijeruhi nilimwona mkononi akiwa ameshika kisu kidogo cha kukunja, alinikamata roba ya shingo na kuniambia kwa ukali shuka kwenye pikipiki huku akiwa amechomoa funguo ya pikipiki yangu”

“Baada ya mimi kushuka kwenye pikipiki, huku akiwa amenishika roba alikuwa akinivuta kuelekea kituo kidogo cha polisi kilichopo pale stendi, nikaingia ndani ya kile kituo na kuniambia piga magoti, nilipopiga magoti ndipo nikaona ameshika hicho kisu na kunichoma nacho kichwani na damu zikaanza kutoka kwa wingi ambapo askari mmoja niliyemtambua kwa jina moja la Seifu ndiye aliyenichukua na kunikimbiza hospitali kwa matibabu zaidi”, alisema Erick Shonga.

Mkuu wa wilaya anena:

Katika hatua nyingine Mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga, alipozungumza kwa njia ya simu na mwandishi wa habari hizi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa, wakati waendesha pikipiki hao wanaandamana kuelekea kituo cha polisi yeye alichukua maamuzi ya kwenda kuzungumza nao na kuwatuliza wasiwe na jazba wakati serikali inalifanyia kazi tatizo hilo.

“Tutakaa kikao kujadili suala hili ili tuone tunachukua maamuzi gani, kwa sasa siwezi kuzungumzia lolote mpaka tukae tuone hali ilikuaje lakini ninachoweza kukuambia hapa huyu dereva wa pikipiki aliyejeruhiwa amepewa PF 3 na yupo hospitali anapatiwa matibabu”, alisema Ngaga.

Kamanda wa Polisi athibitisha:

Naye Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela alipozungumza na Mtandao huu alisema askari aliyefanya kitendo hicho aliwekwa mahabusu katika kituo kikuu cha polisi wilayani Mbinga, na kwamba limefunguliwa jalada la uchunguzi kwa hatua zaidi juu ya tukio hilo.

“Nyandindi hapa nasubiri jalada la uchunguzi lililetwe hapa mkoani ili tuweze kuanza kazi ya kuchunguza tukio hili, kazi hii itakapo kamilika tutatoa taarifa kamili”, alisema Msikhela.

No comments: