Wednesday, October 1, 2014

IDADI YA WALIOKUNYWA TOGWA YENYE SUMU WAONGEZEKA


Na Muhidin Amri,
Songea.


IDADI ya watu walioathirika kutokana na kunywa kinywaji aina ya togwa ambacho kinasadikiwa kuwa na sumu, katika kijiji cha Litapaswi kata ya Mpitimbi wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, imeongezeka kutoka 250 na kufikia watu 325.

Akizungumza na Waandishi wa habari mjini hapa, Kamanda wa Polisi wa mkoa huo Mihayo Msikhela alisema tukio ilo limetokea juzi katika kijiji hicho, wakati watu hao wakiwa kwenye sherehe ya kipaimara ya mwanafunzi wa darasa la sita Dickson Nungu ambaye anasoma  shule ya msingi  Litapwasi.

Kamanda Mihayo alifafanua kuwa kati ya waathirika hao watu 29 wamelazwa katika hospitali ya misheni Peramiho, ambapo kati yao wanaume wapo wane na wanawake 22.


Aidha watoto wapo watatu huku wengine 295 wamefikishwa katika zahanati ya Lyangweni ambao  wanaume ni 118, wanawake 148 na watoto 29.

Katika waathirika hao tayari wengine 225 wameshatibiwa na kuruhusiwa  huku watu 71 bado wanaendelea kupatiwa huduma katika kituo cha matibabu kilichopo shule ya msingi Kiwalawala.
 
Kufuatia tukio hilo watu watano wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma kuhusiana na tukio hilo, ambapo kwa mujibu wa Kamanda Mihayo aliwataja wanaoshikiliwa kuwa ni Ernest Nungu, Benedict Nungu Esebius Komba, Sadik Masoud na John Kaulangudidi wote wakazi wa  kijiji cha Litapwasi.

No comments: