Saturday, October 4, 2014

SHULE YAKOSA VYOO KAMATI YA UJENZI LAWAMANI

Baadhi ya watoto wa shule ya msingi Mbambi wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wakiwa kwenye ukumbi wa Umati mjini hapa wakishuhudia kufanyika kwa tendo la mahafali kwa wanafunzi wenzao, ambao wamehitimu darasa la saba. (Picha na Kassian Nyandindi)

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

KAMATI ya ujenzi shule ya msingi Mbambi wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, imetakiwa kuchukua hatua za haraka juu ya ujenzi wa vyoo katika shule hiyo ili kuwafanya wanafunzi, waweze kuondokana na tatizo la kupanga foleni pale wanapohitaji kujisaidia.

Aidha imeshushiwa lawama kwa kuzembea kutekeleza suala hilo huku ikielezwa kuwa mahitaji ya vyoo katika shule hiyo ni matundu 18 lakini yaliyopo sasa ni nane tu, ambayo hutumia wanafunzi hao na kufanya tatizo hilo kuwa kero miongoni mwao.

Hayo yalisemwa na Gerold Ndunguru alipokuwa mgeni rasmi katika mahafali ya darasa la saba shule ya msingi Mbambi, yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Umati uliopo mjini hapa.

“Ndugu zangu hii ni aibu kwa shule hii ambayo ipo hapa Mbinga mjini kusikia haina vyoo, napenda kusisitiza kamati ya ujenzi ione umuhimu juu ya jambo hili kupewa kipaumbele na namna gani inashirikisha wazazi kwa karibu katika kutatua kero hii”, alisema Ndunguru.

Ndunguru alifafanua kuwa mazingira ya kusomea mtoto wakati wote inatakiwa yawepo katika hali nzuri, na kwamba suala la kufumbia macho tatizo hilo wakati watoto hao wanapata shida ni dhambi.

Pamoja na mambo mengine akizungumzia suala la wazazi kupeleka watoto wao shule, alisisitiza wajiwekee akiba kidogo kidogo na sio kusubiri mtoto amefaulu ndipo mzazi anaanza kuhangaika kutafuta fedha, jambo ambalo alisema ni uzembe mkubwa.

“Hakuna dhambi kubwa wazazi wenzangu kama umeweza kumleta mtoto duniani halafu ukamnyima elimu, tendo hili tunalolifanya hapa leo ni msingi wa maendeleo ya maisha ya watoto hawa na linaleta furaha”, alisema.

Awali Mwenyekiti wa shule hiyo Wolfgan Komba, akitoa maelezo mafupi juu ya shule ya msingi Mbambi alieleza kuwa jitihada za walimu kufundisha darasani maendeleo yake ni mazuri na kwamba, mfumo wa matokeo makubwa sasa (BRN) shule hiyo ni moja kati ya shule za wilaya ya Mbinga ambazo zimeweza kupata cheti kwa kufanya vizuri.

 


No comments: