Wednesday, October 1, 2014

WASHUSHIWA KIPIGO NA KUFARIKI DUNIA



Na Mwandishi wetu,
Ruvuma.

WATU wawili kati ya watatu ambao majina yao hayajafahamika hadi sasa mjini hapa, wanaodaiwa kuwa ni wezi  wamefariki dunia baada ya kushushiwa kipigo na wananchi wenye hasira kali, wakati wakiiba pikipiki.

Wezi hao walikamatwa wakiiba pikipiki tatu zenye namba za usajili T 5888 CJC, T363 BFL na T445 CJT zote aina ya Sanlg.

Katika tukio hilo wezi hao walimjeruhi kwa nondo  Vasco Dagama fundi pikipiki mkazi wa Matogoro Manispaa ya Songea na kumnyanganya pikipiki yenye namba za usajili T363 BFL aina ya Sanlg.


Kwa mujibu wa Kamanda  wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela alisema baada ya watu hao kufanikisha uporaji huo Dagama alipiga kelele ya kuomba msaada, ndipo kundi kubwa la watu lilipojitokeza na kuanza kuwashambulia watu hao ambapo mmoja kati ya hao alinusurika kifo baada ya kukimbia, na wawili walipigwa hadi kufa.

Miili yao imehifadhiwa katika chumba cha maiti hospitali ya mkoa Songea huku Jeshi la polisi mkoani humo, likiendelea na uchunguzi kuhusiana na tukio hilo.

Hata hivyo Jeshi hilo limewataka wananchi kuacha tabia ya kujichukulia  sheria mkononi wakati matukio ya aina hiyo yanapojitokeza, badala yake wawafikishe watuhumiwa katika vyombo vya sheria au kutoa taarifa polisi.

No comments: